IQNA

Al Azhar yakaribisha uanachama wa Palestina UNESCO

12:58 - November 03, 2011
Habari ID: 2216863
Ahmad Tayyib, Sheikh wa chuo cha kidini cha al-Azhar amekaribisha kupewa uanachama kamili Palestina katika Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO.
Kwa mujibu wa gazeti la Misri la al-Yaum as-Sabi' Sheikh Ahmad Tayyib amesema kuwa uanachama huo wa Palestina ni ushindi wa haki dhidi ya batili na kwamba ni matunda ya Wapalestina kufuata sera za amani na kujitolea. Amesema huo ni mwanzo wa Palestina kutambulika rasmi kama nchi inayojitawala katika Umoja wa Mataifa.
Sheikh Tayyib amesema kuwa leo ulimwengu unatambua vyema kiwango cha dhulma inayotekelezwa na utawala dhalimu wa Israel dhidi ya taifa la Palestina na kwamba hivi sasa wakati umewadia wa kuundwa serikali moja na rasmi nchini Palestina.
Amesifu juhudi za nchi za Kiislamu na Kiarabu za kupigania uanachama wa Palestina katika shirika la UNESCO na kutaja msimamo wa nchi za Kiafrika, Latin Amerika na Ufaransa za kuunga mkono juhudi hizo kuwa ni wa kujivunia.
Sheikh wa al Azhar amezitaka Marekani na nchi nyingine za Magharibi zinazounga mkono utawala haramu wa Israel kutambua kwamba suala la Palestina ndilo suala lililo na umuhimu mkubwa katika ulimwengu wa sasa na amezihimiza kufanya juhudi za kulitatua suala hilo badala ya kuweka vikwazo katika juhudi za kimataifa za kulitafutia suluhisho la kudumu.
Vilevile amezitaka nchi hizo na hasa Marekani na Canada zilizopinga wazi wazi uanachama wa Palestika katika shirika la UNESCO kuweka kando siasa zao za kindumakuwili kuhusiana na ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu na kufanya juhudi za kukomesha dhulma ya wazi ya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina.
Amemaliza kwa kusema kuwa uungaji mkono mkubwa wa kimataifa kwa suala la Palestina kujiunga na UNESCO ni ishara ya wazi inayothibitisha kwamba ulimwengu sasa umechukua mkondo tofauti wa kuhudumia masuala ya kibinadamu na mataifa yamayodhulimuwa duniani. 892034
captcha