Yusuf al Ahmad, Mjumbe wa Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu amesema kuwa, uamuzi huo wa kusimamishwa uanachama wa Syria unakiuka wazi wazi mkataba wa jumuiya hiyo.
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imetangaza kusimamisha uanachama wa Syria katika jumuiya hiyo jana na kutoa wito wa kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na kisiasa nchi hiyo ya Kiarabu. Vilevile imezitaka nchi za Kiarabu kuwaita mabalozi wao kutoka Syria.
Uamuzi huo umechukuliwa katika kikao cha dharura kilichofanyika jana katika mji mkuu wa Misri, Cairo. Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imesema kuwa, imelazimika kuchukua hatua hiyo kutokana na kushindwa serikali ya Rais Bashar al Assad kusitisha machafuko nchini humo kufikia Novemba 2 kama ilivyotakiwa.
Katika hali ambayo upinzani umekuwa ukivituhumu vyombo vya usalama vya Syria kuwa vinatumia nguvu kupita kiasi kukabiliana na waandamanaji, serikali ya Damascus imekuwa ikisisitiza kuwa, magenge ya wabeba silaha yenye kuungwa mkono na nchi za kigeni ndiyo yanayochochea machafuko nchini humo.
Wakati huo huo Wananchi wa Syria wamevamia ofisi za balozi za Saudi Arabia na Qatar mjini Damascus kulaani hatua ya nchi hizo kuongoza hatua ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kusimamisha uanachama wa Syria.
Aidha waandamanaji wenye hasira Syria wameandamana nje ya ubalozi wa Marekani. Wananchi wa Syria wanasema Marekani imezichochea nchi za Kiarabu dhidi ya Syria.
897484