IQNA

Wasyria wa Lebanon waandamana kumuunga mkono Rais Bashar Assad

11:45 - November 14, 2011
Habari ID: 2222395
Wasyria wanaoishi nchini Lebanon wameandamana mbele ya ubalozi wa nchi yao mjini Beirut wakilaani uamuzi uliochukuliwa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wa kusimamisha uanachama wa Damascus kwenye jumuiya hiyo.
Waandamanaji hao walikuwa wamebeba picha za Rais Bashar Assad wa Syria na bendera ya nchi hiyo na kuitaka Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ikomeshe kuingilia mambo ya ndani ya Syria.
Jana pia maelfu ya wananchi wa Syria walimiminika katika barabara za miji muhimu ya nchi hiyo wakilaani hatua ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ya kusimamisha uanachama wa Damascus.
Katika maandamano hayo hususan katika mji mkuu wa Syria Damascus, wananchi wa Syria mbali na kulalamikia uamuzi huo wa Arab League, aidha wameonyesha uungaji mkono wao mkubwa kwa serikali ya Rais Bashar al Assad.
Jumamosi iliyopita Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilisimamisha uanachama wa Syria katika jumuiya hiyo na kutoa wito wa kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na kisiasa nchi hiyo ya Kiarabu. Vilevile imezitaka nchi za Kiarabu kuwaita nyumbani mabalozi wao walioko Syria.
Uamuzi huo ulichukuliwa katika kikao cha dharura kilichofanyika katika mji mkuu wa Misri, Cairo.
Yusuf al Ahmad, Mjumbe wa Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu alisema kuwa, uamuzi huo wa kusimamishwa uanachama wa Syria unakiuka wazi wazi mkataba wa jumuiya hiyo na umechukuliwa kwa misingi ya kisiasa. 898267
captcha