IQNA

Wazayuni waeneza chuki dhidi ya Uislamu na Iran barani Afrika

14:22 - November 20, 2011
Habari ID: 2225075
Utawala wa Kizayuni wa Israel unajaribu kuanzisha ushirikiano na baadhi ya nchi za Afrika kwa lengo la kuupiga vita Uislamu na ushawishi wa Iran barani Afrika.
Kwa mujibu wa gazeti la Al Akhbar la Misri likinukulu gazeti la Kizayuni la Maariv, Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu hivi karibuni alifanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa Afrika ili kubuni muungano huo bandia.
Ripoti hiyo inasema Netanyahu hivi karibuni alikutana na Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga na Rais Yoweri Museveni wa Uganda kujadili suala hilo. Miezi michache iliyopita alikutana pia na rais wa nchi mpya ya Sudan Kusini pambizoni mwa kikao cha Umoja wa Mataifa mjini New York.
Hivi karibuni kiongozi mwandamizi wa Utawala wa Kizayuni wa Israel alisema kuwa kuenea Uislamu barani Afrika kunazitia hofu nchi alizozitaja kuwa za Kikristo barani Afrika.
Tayari njama hizo za utawala wa Kizayuni zimekabiliwa na radiamali kali nchini Kenya.
Waziri wa Ulinzi wa Kenya Yusuf Haji amepinga hatua ya Waziri Mkuu Raila Odinga kwenda Israel na kuomba msaada wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni katika vita dhidi ya al Shabaab.
Haji amesema msimamo wa Odinga alipokutana na Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu ‘yamkini ulikuwa msimamo binafsi'. Ameongeza kuwa safari ya Odinga Israel wiki iliyopita haikuwa katika strategia ya Kenya ya kutafuta msaada wa kimataifa kuhusu Somalia.
Haji amesema kuhusu kadhia ya Somalia kuwa, Kenya inashirikiana tu na taasisi za kimataifa kama vile IGAD, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa.
Waasi wa Al Shabaab sasa wanasema Odinga alikuwa Israel kutafuta msaada wa kuangamiza Waislamu na Uislamu Somalia. Yusuf Haji amekanusha madai hayo na kusema vita vya Somalia si vya kidini bali ni mapambano dhidi ya kundi la kigaidi linalotishia usalama wa kieneo na kimataifa. Jeshi la Kenya liliingia Somalia zaidi ya mwezi moja uliopita kwa lengo la kuwaangamiza waasi wa al Shabaab.
Njama za utawala wa Kizayuni za kupiga vita Uislamu na ushawishi wa Jamhuri ya Kiislamu barani Afrika zitafeli. Ni wazi kuwa utawala wa Kizayuni unatapatapa katika kipindi hiki cha kuenea wimbi la mwamko wa Kiislamu duniani.
900209
captcha