IQNA

Saudi Arabia yavunja haki za Waislamu wa Kishia

16:35 - November 23, 2011
Habari ID: 2227214
Katika hali ambayo vuguvugu la mapinduzi ya wananchi wa nchi za Kiarabu likiwa linashuhudiwa pia Saudi Arabia, viongozi wa nchi hiyo ambao wanavunja waziwazi haki za binadamu za raia wao, wamewafukuza wananchi 108 ambao ni Waislamu wa madhehebu Kishia nchini humo.
Tovuti ya habari ya al Mustaqbal al Arabiya imefichua kuwa, Waislamu hao waliofukuzwa wamesafirishwa nje ya Saudi Arabia kwa ndege za shirika la ndege la Qatar. Viongozi wa Saudia wamechukua hatua hiyo isiyo ya kiutu katika hali ambayo, machafuko yalishuhudiwa katika siku za hivi karibuni kwenye maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo. Mikoa ya al Sharqiya na Qatif ni miongoni mwa mikoa ya Saudia ambayo sambamba na kuanza wimbi la mwamko wa Kiislamu katika nchi nyingi za Kiarabu, nayo pia imeshuhudia malalamiko ya wananchi Waislamu wa Kishia na wengineo ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakidhulumiwa haki zao nchini humo.
Waislamu wa Kishia wa Saudia licha ya kuwa wanaunda asilimia 15 ya wananchi wa nchi hiyo, lakini hawapati haki sawa kama wananchi wengine wa nchi hiyo.
Ukweli ni kuwa Waislamu hao wa madhehebu ya Shia Saudia wanahesabiwa kuwa raia wa daraja la pili na pia wanashirikishwa kwa uchache katika kazi na taasisi mbalimbali za serikali. Vilevile mfumo wa kisiasa wa Saudi Arabia huwawekea Waislamu wa Kishia wa nchi hiyo vikwazo katika kufanya hafla na shughuli mbalimbali za kidini.
Uhusiano wa utawala wa Aal Saudi katika kuamiliana na Waislamu wa Kishia nchini humo unaonyesha kuwa unawatazama raia hao kama watu wa kundi fulani na kwa msingi wa madhehebu yao. Mtazamo huo uliotokana na baadhi ya mafundisho yaliyofurutu ada ya itikadi ya Kiwahabi yaliyopenya katika utawala wa Saudia, umepelekea wafuasi wa madhehebu ya Shia waishi katika hali ngumu. Baadhi ya ripoti zimeeleza kuwa, kuna wafungwa 30,000 wa kisiasa nchini humo na wengi sana kati ya wafungwa hao ni Waislamu wa Kishia. Hata imefichuliwa kuwa, ili kuwabana zaidi Waislamu hao, serikali ya Riyadh mwaka huu haikuwapa ruhusa baadhi ya wafuasi wa madhehebu hayo ya Kiislamu kutoka mikoa ya mashariki mwa nchi hiyo kushiriki katika ibada ya Hija. Hatua hiyo imechukuliwa na ukoo wa Kiflme wa Aal Saud huko Saudi Arabia ili Waislamu wa Kishia nchini humo wasiweze kuwasiliana na Waislamu wengine wa nchi mbalimbali duniani.
Katika miezi ya hivi karibuni pia, Waislamu wa Kishia wa Saudia ambao wengi wao wanaishi mashariki mwa nchi hiyo wamekuwa wakiandamana kama wananchi wengine wa nchi za Kiarabu ili kudai haki zao muhimu wanazodhulumiwa. Suala hilo limewakasirisha viongozi wa Riyadh. Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema katika ripoti yake iliyochapishwa wiki mbili zilizopita kwamba, wanaharakati 160 wa kisiasa wametiwa mbaroni katika kipindi cha miezi 8 iliyopita nchini Saudi Arabia. Nukta ya kuzingatia hapa ni kuwa wengi miongoni mwa waliotiwa mbaroni ni Waislamu wa Kishia. Lakini ukweli ni kuwa mabadiliko yanayoshuhudiwa hivi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati yanasonga mbele na hayawezi kukwamishwa na vitendo vya ukandamizaji na uonevu vya watawala madikteta. Hii ni kwa sababu wananchi wa eneo hili hasa wale wanaodhulumiwa wanaendelea kupaza sauti zao na kupigania matakwa yao bila kujali tofauti zao za kidini na kikabila wala kuogopa watawala wanaotumia mabavu. Na suala hili linawatia hofu na kihoro zaidi watawala wa nchi kama vile Saudi Arabia na Jordan ambazo ndizo zinazoongozwa zaidi na tawala za kifalme za kurithishana kuliko nchi nyingine.
903222
captcha