Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Iran amepuuza madai ya Saudi Arabia dhidi ya Tehran kwamba, inaingilia masuala ya ndani ya nchi za Mashariki ya Kati na kusisitiza kwamba, madai hayo ni ya kushangaza na kusikitisha mno.
Ramin Mehmanparast ameeleza kushangazwa mno na madai hayo na kubainisha kwamba, Tehran inataraji kuwaona viongozi wa Riyadh wakirekebisha siasa zao za kivitendo mkabala na Iran na nchi za Mashariki ya Kati badala ya kushikilia tuhuma kama hizi zisizo na kichwa wala miguu.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Iran amewataka viongozi wa Saudi Arabia kuitikia wito na matakwa halali ya wananchi wake badala ya kujihusisha na tuhuma kama hizi ambazo hazina lengo jingine ghairi ya kuwafaidisha maadui.
Mehmanparast ameashiria pia suala la miradi ya nyuklia ya Tehran kuwa ni kwa ajili ya malengo ya amani na kusema, daima Tehran imekuwa ikisisitiza juu ya suala la kusafishwa ulimwengu na silaha za nyuklia.
906712