IQNA

Utawala wa Bahrain washambulia wanawake waombolezaji wa Muharram

15:56 - November 28, 2011
Habari ID: 2230594
Vibaraka wa utawala wa Aal Khalifa wa Bahrain wameshambulia kundi moja la wanawake waliokuwa wakiomboleza katika usiku wa kwanza wa mwezi huu wa huzuni wa Muharram, kwa kutumia gesi za kutoa machozi na mabomu ya sauti.
Tukio hilo la kinyama dhidi ya wanawake wa Kishia lilitekelezwa na vibaraka hao siku ya Jumamosi usiku. Baada ya kushambulia kundi hilo la wanawake waombolezaji katika mtaa wa Aali, askari hao vibaraka walimtia nguvuni Zeinab al-Khoja mwanaharakati wa Bahrain.
Askari hao waliendeleza hujuma yao dhidi ya waombolezaji kwa kuvamia vijiji vingine vya karibu na kuzusha hofu na wasiwasi mkubwa miongoni mwa wakazi wa vijiji hivyo. Askari wa Bahrain wanaosaidiwa na askari vamizi wa Saudi Arabia wamekuwa wakitekeleza vitendo vya ukandamizaji na mashinikizo dhidi ya Mashia wa nchi hiyo wanaopigana dhidi ya dhulma ya ufalme wa Bahrain.
Kinyume na ilivyo katika nchi nyingine za Kiarabu zinazoshuhudia harakati za mapinduzi dhidi ya madikteta wa nchi hizo, harakati za Waislamu wa Bahrain zimesahaulika na kupuuzwa kabisa na mashirika ya habari pamoja na jamii ya kimataifa inayodai kutetea haki za binadamu na demokrasia. 905945
captcha