Vyombo vya serikali ya Iraq vimekadiria kuwa Waislamu milioni saba wameshiriki katika shughuli ya jana ya maombolezo ya kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume katika mji mtakatifu wa Karbala.
Hapa nchini Iran miji mbalimbali ilifurika kwa mamilioni ya Waislamu walioshiriki katika maombolezo ya kuuawa shahidi Imam Hussein, Ahlubaiti na masahaba zake 72 waliouawa na jeshi la Yazid bin Muawiya mwaka 61 Hijria.
Maombolezo kama hayo yameshuhudiwa pia katika nchi nyingi za Kiislamu na zisizokuwa za Kiislamu ambapo Waislamu hususan wafuasi wa madhehebu ya Shia wamekumbuka tukio la kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad Imam Hussein (as) jamaa na masahaba zake.
Nchini Tunisia pia jana na baada ya miaka mingi walihuisha siku ya Ashura na kuomboleza mauaji ya Imam Hussein baada ya kuzuiwa kwa miaka mingi na utawala wa kidikteta uliong'olewa madarakani wa Zainul Abidin bin Ali. Washiriki katika maombolezo hayo ya Tunisia walikuwa na hisia mchanganyiko za huzuni kubwa ya kukumbuka tukio la kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume (saw) kwa upande mmoja, na furaha ya kuruhusiwa tena kuhuisha siku ya Ashura na kuwakumbuka Watu wa Nyumba ya Mtume waliouawa kinyama mwaka 61 Hijria katika ardhi ya Karbala.911457