IQNA

Saudi Arabia; mwenyeji wa kikao cha Mawaziri wa Utamaduni

15:21 - December 21, 2011
Habari ID: 2242698
Katibu Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ISESCO, amesema kuwa kikao cha nane cha Mawaziri wa Utamduni wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu OIC kitafanyika nchini Saudi Arabia.
Katibu Mkuu wa ISESCO Abdul Aziz at-Tuweijri, amesema kwamba katika kikao chao cha saba kilichomalizika hivi karibuni nchini Algeria, Mawaziri wa Utamaduni wa OIC wameafikiana kwamba kikao chao cha nane kifanyike nchini Saudia mwaka 2013.
Akizungumzia suala hilo Abdullah al-Jasir, Waziri wa Utamaduni na Habari wa Saudi Arabia amesema kuwa nchi yake ilitoa ombi la kutaka kikao hicho kifanyike nchini kwake mwaka uliotajwa kutokana na kuwa mwaka huohuo mji mtakatifu wa Madina utakuwa unafanya maadhimisho ya kuteuliwa mji huo kuwa mji mkuu wa utamaduni wa Ulimwengu wa Kiislamu. Katika kikao chao cha saba mjini Algiers, Algeria, Mawaziri wa Utamaduni wa Nchi za Kiislamu walisisitiza kufuatiliwa juhudi za kuboresha maisha ya Waislamu na kusahihisha fikra mbovu zinazotawala ulimwenguni kuhusiana na Uislamu na Waislamu.
Haja ya kushirikiana mataifa tofauti ya Kiislamu kwa maslahi ya umma wa Kiislamu ni jambo lililosisitizwa kwenye kikao hicho. Matokeo mengine muhimu yaliyopatikana katika kikao cha Algeria ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupewa uenyeji wa kikao cha 10 cha ISESCO mwaka 2017 ambapo mwaka huohuo mji mtakatifu wa Mash'had pia umechaguliwa kuwa mji mkuu wa kiutamaduni wa Ulimwengu wa Kiislamu. 919911
captcha