Kwa mujibu wa gazeti la al-Intiqad linalochapishwa Lebanon, maandamano hayo yaliyofanyika chini ya anwani ya 'Kutetea Misikiti Iliyoharibiwa' yaliitishwa na Baraza la Wanazuoni wa Kishia wa Bahrain. Ayatullah Isa Qassim, Kiongozi wa Mashia wa Bahrain na wanazuoni kadhaa mashuhuri wa nchi hiyo pia walishiriki katika maandamano hayo katika Msikiti wa Imam Swadiq mjini Manama.
Baraza lililotajwa la wanazuoni lilitoa taarifa mwishoni mwa maandamano hayo likisema kuwa watu wanaohusika na ubomoaji na uchomaji wa misikiti na wakati huohuo kuwazuia waumini kuingia katika maeneo hayo ya ibada watawajibika mbele ya Mwenyezi Mungu na historia. Taarifa hiyo imesisitiza juu ya udharura wa kukarabatiwa na kujengwa upya misikiti iliyoharibiwa na kuongeza kuwa utukufu wa maeneo hayo hauwezi kupotea hata kama yatabomolewa na kusawazishwa na ardhi.
Ayatullah Isa Qassim amekemea vikali kimya cha mashirika na taasisi za kutetea haki za binadamu duniani mbele ya jinai zinazotekelezwa na utawala wa Aal Khalifa dhidi ya Wabahraini na hasa wanawake wanamapinduzi wa nchi hiyo. Amesekitishwa mno na msimamo wa taasisi hizo ambazo amesema hadi leo hazijatambua rasmi kwamba taifa la Bahrain ni miongoni mwa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu yanayopigania haki zao za kimsingi kabisa. 921458