IQNA

Hizbullah yalaani vikali njama za utawala wa Kizayuni za kuvuruga historia

14:13 - December 27, 2011
Habari ID: 2246121
Chama cha Hizbullah cha Lebanon kimelaani vikali njama za utawala wa Kizayuni wa Israel za kutaka kuugeuza mji wa Quds kuwa mji mkuu wake.
Utawala wa Kizayuni umepeleka muswada Bungeni ambapo kama utapitishwa, basi mji wa Baytul Muqaddas wenye kibla cha kwanza cha Waislamu utatangazwa kuwa mji mkuu wa Israel.
Taarifa iliyotolewa jana usiku na chama cha Hizbullah cha Lebanon imelaani vikali muswada huo hususan kutokana na historia ya Bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel ya kupitisha sheria mbalimbali za kibaguzi na kidhulma.
Hizbullah imesema katika taarifa yake hiyo kuwa, kitendo hicho cha Wazayuni ni uvunjaji wa wazi wa haki za Wapalestina.
Waislamu pamoja na wananchi wa Palestina wanauhesabu mji wa Baytul Muqaddas kuwa ni mji mkuu kihistoria wa nchi taifa la Palestina, lakini utawala wa Kizayuni unafanya kila njia ili kupotosha historia na kuuyahudisha mji huo mtukufu.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushiriano wa Kiislamu naye pia amezungumzia suala hilo na kusisitizia juu ya udharura wa kukabiliana na mpango wa Kizayuni wa "Quds Mji Mkuu wa Taifa la Kiyahudi".
Profesa Ekmeleddin Ihsanoglu Katibu Mkuu wa OIC jana alitoa taarifa rasmi kuhusiana na kadhia hiyo ambapo sanjari na kulaani muswada wa Wazayuni wa kuitambua Quds kuwa mji mkuu wa taifa la Kiyahudi amesisitiza kuwa, mpango huo ni batili na akazitaka asasi za kimataifa kusimama kidete ili kukabiliana na hatua hiyo.
Taarifa ya Katibu Mkuu wa OIC imebainisha kwamba, kupasishwa kunakotarajiwa kwa mpango huo wa Wazayuni ni hujuma ya moja kwa moja ya Wazayuni kwa matukufu ya Wapalestina pamoja na haki zao zisizo na chembe ya shaka.
Taarifa ya OIC imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Kamati ya Pande Nne ya Mashariki ya Kati na Shirika la Elimu Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuchukua hatua za dhati na za jaddi za kuzuia siasa za kibaguzi za Israel.
923467
captcha