Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imetangaza kwamba kikao cha kimataifa cha kutetea Quds kilichokuwa kimepangwa kufanyika tarehe 16 mwezi huu wa Januari mjini Doha, Qatar sasa kimeakhirishwa na kitafanyika mwezi Februari.
Kwa mujibu wa tovuti ya lopinion, Muhammad Swabih, Naibu Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo anayeshughulikia masuala ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel, amesema mbele ya waandishi habari kwamba uamuazi wa kuakhirisha kikao hicho umetokana na ombi la serikali ya Qatar. Amesema kikao hicho sasa kimepangwa kufanyika tarehe 25 hadi 27 za mwezi ujao wa Februari.
Muhammad Swabih amesema katika sehemu nyingine ya matamshi yake kwamba kikao hicho kimepangwa kujadili masuala tofauti kama vile, Quds na sheria za kimataifa, Quds na njia za kukabiliana na uchokozi wa utawala wa Kizayuni, kupambana na njama za kuyahudisha maeneo ya Kiislamu na nafasi ya jumuiya za kiraia katika kulinda Quds.
Amesema Jumuiya ya Nchi za Kiarabu itatumia kikao hicho kuzishawishi jumuiya za kiraia na zisizo za kiraia kulinda Quds na kuzuia kuendelea ujenzi wa vitongoji vya Mayahudi katika ardhi za Wapalestina. 926780