IQNA

Mahakama: Mubarak anastahiki mwisho mbaya

19:00 - January 03, 2012
Habari ID: 2250756
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Jinai ya Misri inayosikiliza kesi ya Rais wa zamani wa nchi hiyo Husni Mubarak amesema kuwa dikteta huyo wa zamani anastahiki mwisho mbaya na wenye kudhalilisha kutokana na jinai alizotenda.
Wakati wa kuendelea kusikilizwa kwa kesi ya mtawala huyo wa zamani wa Misri baada ya kuakhirishwa kwa miezi mitatu hii leo mjini Cairo, Mustafa Suleiman amesema kuwa, Mubarak alifanya kila awezalo katika miaka 10 ya mwisho ya utawala wake kuhakikisha kuwa anamrithisha mwanawe kiti hicho. Suleiman amesema kuwa, dikteta huyo wa zamani anastahiki hukumu kali kwa kufanya dhuluma na kuongoza taifa hilo la kaskazi mwa Afrika kwa ngumi ya chuma.
Mubarak, wanawe wawili wa kiume Alaa na Jamal pamoja na Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani Habib al Adly wanakabiliwa na mashtaka ya kula rushwa, ubadhirifu wa fedha za umma na kuhusika na mauaji ya raia wakati wa vuguvugu la mapinduzi ya nchi hiyo, lililopelekea kuanguka kwa utawala wa dikteta huyo mwezi Februari mwaka jana. 928249

captcha