Amesema Iran inapinga kuwepo vikosi vya kigeni katika eneo la Ghuba ya Uajemi .
Matamshi hayo ya Waziri wa Ulinzi yanakuja punde baada ya onyo kali la Kamanda wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa manowari ya kivita yenye kusheheni ndege ya Marekani limepelekea wakuu wa Washington kutoa jibu.
Baada ya kumalizika mazoezi makubwa ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yaliyopewa jina la 'Velayat 90' katika eneo la Bahari ya Oman na Kaskazini mwa Bahari ya Hindi, Meja Jenerali Ataullah Salehi Kamanda wa Jeshi la Iran ameashiria kuondoka Ghuba ya Uajemi manowari ya kivita yenye kusheheni ndege ya Marekani na kuionya manoari hiyo kuwa isirejee sehemu yake ya awali katika Ghuba ya Uajemi kwani mara hii Iran haitatosheka tu na kutoa onyo.
Kufuatia onyo hilo, George Little Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, amesema nchi hiyo haitaki kukwaruzana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. George Little ameeleza kuwa hakuna kiongozi yoyote wa White House mwenye lengo la kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika lango la Hormoz. Amedai kuwa vikosi vya majini vya Marekani viko katika eneo la Ghuba ya Uajemi kwa msingi wa sheria za kimataifa. Little ameendelea kudai kuwa manowari inayobeba ndege za kivita za Marekani na manowari zingine zinazoandamana nayo ziko katika Guba ya Uajemi na Lango la Hormoz kwa mujibu wa mikataba ya kiusalama.
Sambamba na maneva za jeshi la wanamaji la Iran, manowari inayobeba ndege ya kivita ya Marekani ijulikanayo kama USS John C Stennis iliondoka eneo la Lango la Hormoz katika Ghuba ya Uajemi.
Katika miaka yote ya kukaliwa kwa mabavu Iraq, manoari za kivita zenye kusheheni ndege za Marekani zimekuwepo katika Ghuba ya Uajemi na maji ya kieneo kwa lengo la kuunga mkono oparesheni za kijeshi za Marekani nchini Iraq. Kwa kuzingatia umuhimu wa kistratijia wa eneo la Ghuba ya Uajemi hasa kwa mtazamo wa vyanzo vingi vya mafuta ya petroli na gesi, manowari za kivita za Marekani zimekuwepo katika eneo hili tokea zama za vita baridi. Baada ya kumalizika vita vya pili vya Ghuba ya Uajemi Marekani iliendelea kubakisha manoari zake hizo kwa madai ya kudhamini usalama wa eneo katika fremu ya mikataba na baadhi ya nchi za Ghuba ya Uajemi. Hivi sasa Marekani ina vituo vya kijeshi huko Saudi Arabia, Qatar, Bahrain, Imarati, Oman na Kuwait kwa lengo la kudumisha ubabe wake wa kijeshi katika eneo hili.
Katika miaka ya hivi karibuni Marekani imeanzisha mradi wa kipropaganda wa 'chuki dhidi ya Iran' na kwa njia hiyo kuzichochea nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi kununua idadi kubwa ya silaha kwa lengo la kukabiliana na kile kinachodaiwa eti ni tishio la Iran. Mbali na kuibua mashindano ya ununuzi wa silaha Marekani pia imetumia fursa hiyo kuongeza idadi ya vikosi vyake katika Ghuba ya Uajemi. Hii ni katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama nchi yenye pwani ndefu zaidi yenye kilomita karibu 2000 katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman imekuwa ikisisitiza udharura wa kudhamini usalama wa eneo kwa kutegemea vikosi vya mataifa ya eneo hili. Katika uhusiano wake na majirani zake, Iran imekuwa ikijitahidi kudumisha amani, uthabiti, na ujirani mwema kama sera yake ya kigeni ya kistratijia. Mazoezi ya kijeshi ya Iran katika eneo yalikuwa na ujumbe huu kuwa, vikosi vya nchi za Ghuba ya Uajemi kwa mshikamano vinaweza kudhamini usalama wa eneo. Kwa hakika, kuwepo vikosi vya kigeni katika eneo hili badala ya kuleta amani katika Ghuba ya Uajemi kunazusha hitilafu, vita na kupotea utajiri kupitia ununuzi wa silaha za nchi za Magharibi. Hakuna shaka kuwa kuwepo vikosi vya kigeni katika eneo la Ghuba ya Uajemi hasa vikosi vya Marekani kunazidisha uwezekano kuibuka vita jambo ambalo ni tishio kwa usalama wa nchi zote.
929246