Kwa mujibu wa gazeti linalochapishwa nchini humo la as-Sha'b, Muhammad Miftah mmoja wa wanachama wa kamati ya waasisi wa chama hicho amesema katika shehere ya uzinduzi wa chama hicho iliyofanyika katika Medani ya Tahrir mjini Sanaa kwamba chama hicho ndicho cha kwanza kinachoungwa mkono moja kwa moja na wananchi. Amesema Chama cha Umma kina mpango madhubuti wa kubuni mfumo wa utawala wa kisiasa nchini Yemen na kwamba lengo lake kuu ni kuunda serikali huru na inayojitawala inayoweka kando aina zote za mifungamano ya kigeni.
Katika taarifa yao ya kwanza, waasisi wa chama hicho wamesema kuwa kimeundwa kwa kushirikisha idadi kubwa ya maulamaa, wanafikra, wanazuoni, wanasiasa, wataalamu wa masuala ya kijamii, wahadhiri na vilevile vijana wanamapinduzi wa Yemen.
Taarifa ya Chama cha Umma inasema kwamba chama hicho ni nembo halisi ya uadilifu, uhuru, usawa na mapambano dhidi ya dhulma na uonevu. Imesema tatizo kuu la nchi hiyo ni uingiliaji wa kigeni na kuwa moja ya malengo makuu ya chama hicho ni kubuni mfumo huru wa utawala usiotegemea uingiliaji wa kigeni. 930206