Taarifa iliyotolewa na seneti hiyo imesema kuwa kufuatia upinzani mkali ulioonyeshwa na Jumuiya ya Kupambana na Chuki dhidi ya Uislamu na Baraza la Waislamu la Ufaransa kwa upande mmoja na ombi la baadhi wa Maseneta kuhusiana na umuhimu wa kufanyiwa marekebisho baadhi ya vipengee vya muswada wa sheria hiyo kwa upande wa pili, Seneti imechukua uamuzi wa kujadili suala hilo tarehe 16 Januari na kisha kulipigia kura siku moja baadaye yaani tarehe 17.
Baadhi ya Maseneta wa Ufaransa ambao kimsingi ni wenye misimamo ya kupindukia mipaka kutoka chama cha mrengo wa kushoto cha kisoshalisti wameazimia kupiga marufuku vazi la hijabu katika shule za kawaida na za chekechea pamoja na maeneo ya burudani kwa kisingizio cha kutoruhusiwa nembo za kidini katika maeneo ya umma.
Jumuiya ya Kupambana na Chuki dhidi ya Uislamu ya Ufaransa imelaani muswada huo na kusema kuwa ni aina ya ubaguzi dhidi ya akina mama wa Kiislamu ambao kwa njia moja au nyingine hulazimika kuandamana na watoto wao wadogo katika shule za chekechea na vilevile katika maeneo ya burudani ya umma.
Wakati huohuo Muhammad Musawi, Mkuu wa Baraza la Waislamu la Ufaransa ametoa taarifa akisema kuwa jamii ya Waislamu wa Ufaransa ina wasiwasi mkubwa kuhusiana na mswada huo ambao unapinga moja kwa moja msingi wa uhuru wa kuabudu. Amesema huko ni kukanyaga moja kwa moja haki za wanawake wa Kiislamu wa Ufaransa.
Ameendelea kusema kuwa licha ya baraza hilo kutangaza kuwa liko tayari kushirikiana na seneti kwa ajili ya kurekebisha baadhi ya vipengee vya mswada huo lakini maseneta wamepinga pendekezo hilo na kuendeleza mipango ya kupasisha mswada huo.930821