IQNA

Kongamano la wanawake Waislamu wanahabari laanza Iran

11:03 - January 09, 2012
Habari ID: 2253550
Kongamano la Kwanza la Kimataifa la Waandishi Habari Wanawake Waislamu limeanza Januari 8 mjini Tehran
Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, sherehe za ufunguzi zimejumuisha hotuba ya Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu Iran Dk. Seyyed Mohammad Hosseini na Mkuu wa Masuala ya Wanawake katika Shirika la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu Bi Sediqah Hijazi.
Dk. Hosseini amesema kuwa Qur’ani Tukufu imetukuza nafasi kubwa ya wanawake na kuwaarifisha kama vigezo si tu kwa wanawake bali hata kwa wanaume. Ameongeza kuwa Qur’ani Tukufu inasisitiza kuwa hakuna tafauti kati ya mwanaume na mwanamke katika jitihada kufikia daraja za juu na kumcha Mwenyezi Mungu.
Amesema takwa au kumcha Mwenyezi Mungu ndio msingi wa familia na kuongeza kuwa misingi ya familia katika baadhi ya maeneo imevunjwa kutokana na Wamagharibi kupuuza takwa. Alimaliza hotuba yake kwa kumnukulu Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Khamenei ambaye karibuni hivi alisema kuwa nchi za Magharibi zinapiga kelele sana kuhusu mwanamke lakini hazitaji suala la familia kwani familia ndio nukta yao ya udhaifu.
Kongamano hilo limewaleta pamoja wahariri wa majarida na magazeti kutoka nchi kama vile Argentina, Misri, Russia, Indonesia, Sudan, Kyrgyzstan, Kosovo, Tatarstan, Iraq, Bosnia, Pakistan, Lebanon, Ghana, Thailand, Syria, Tunisia, na Ufaransa.
Kati ya malengo ya kongamano hilo ni kuarifisha majarida na magazeti ya wanawake Waislamu kutoka maeneo yote ya dunia. Aidha waandalizi wa kongamano hilo wana matumaini kuwa washiriki wataweza kuimarisha uwezo na ushirikiano wao ili kuinua kiwango cha vyombo vya habari vya Kiislamu.
Vilevile wasiriki wanajadili masuala kama vile sheria za Kiislamu, hali ya ulimwengu wa Kiislamu, mikakati ya vyombo vya habari vya Kimagharibi, matukio ya sasa duniani na jukumu la Waislamu, ubepari duniani na jukumu la Waislamu kuhusu ‘Harakati ya Kukalia Wall Street’. Kongamano hilo litaendelea kwa siku saba.
930949
captcha