Hayo yametamkwa na Hashim as-Salman, mwanafikra wa Kishia wa Saudi Arabia ambaye pia ni hatibu wa Msikiti wa Aal ar-Rasul katika mkoa wenye wakazi wengi wa Kishia wa Ihsaa. Amesema nara na maombolezo hayo yamekuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha utambulisho wa Mashia duniani. Amesema maombolezo hayo ni ya pekee ambayo hayana vizuizi wala mipaka ya kijiografia na zama.
Hashim as-Salman ameongeza kuwa maombolezo hayo yanahuishwa kwenye misikiti, nyumba, husseiniya, mashamba na hata kwenye jela kwa sababu hayana mipaka ya wakati wala sehemu. Ameashiria kuhuishwa kwa maombolezo hayo katika kipindi cha miaka mingi iliyopita na kusema kuwa licha ya kuwepo njama za maadui wa Ahlul Bait (as) lakini maombolezo hayo yamekuwa yakifanyika bila kukoma.
Hatibu wa Msikiti wa Aal ar-Rasul nchini Saudi Arabia ameongeza kuwa utawala dhalimu wa dikteta Saddam Hussein wa Iraq ulifanya njama nyingi za kukandamiza na kusimamisha maombolezo hayo lakini haukuweza kuwazuia wananchi Waislamu wa nchi hiyo kuyahuisha.
Sheikh as-Salman amesema kwamba katika zama zilizopita Mashia walijitolea sana katika kulinda Ushia na kwamba leo pia tunashuhudia misafara mirefu ya wapenzi na wafuasi wa Ahlul Bait (as) ikimiminika katika Haram tukufu ya Imam Hussein (as) mjini Karbala, licha ya kuwepo vitisho vingi vinavyohatarisha maisha yao. 931618