IQNA

Kongamano la banki za Kiislamu kufanyika Oman

13:13 - January 10, 2012
Habari ID: 2254586
Taasisi ya Al Ikitisad Wal-Amal ya Oman imeandaa kongamano kubwa la mfumo wa benki na kifedha wa Kiislamu tarehe 23-24 Januari mjini Muscat.
Kwa mujibu wa gazeti la Oman Observer, kongamano hilo ambalo limeandaliwa kwa ushirikiano na Banki Kuu ya Oman litajadili matukio ya hivi karibuni baada ya benki kadhaa nchini kupewa idhini ya kuanzisha huduma za kifedha na kibenki kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu.
Sekta ya benki ya Kiislamu inatazamiwa kukua hadi dola bilioni sita nchini Oman katika kipindi cha miaka mitatu hadi mitano ijayo ambapo kutakuwa na ustawi wa asilimia 8-10.
Masuala muhimu yatakayojadiliwa katika kongamano hilo ni sera na usimamizi wa mfumo wa kifedha wa Kiislamu, ustawi wa benki za Kiislamu katika uga wa kimataifa, mfumo wa fedha wa Kiislamu na masoko ya hisa na nafasi ya mabaraza ya sheria za Kiislamu katika benki.
Kongamano hilo litajumuisha vikao kuhusu utafiti wa hivi karibuni kabisa kuhusu mfumo wa kifedha na benki za Kiislamu.
Inatazamiwa kuwa washiriki 400 kutoka nchi za Kiarabu na Kiislamu wakiwemo wakuu wa mabenki watashiriki katika kongamano hilo.
931851
captcha