IQNA

Jumuiya ya Maulamaa wa Iraq yalaani mlipuko wa kigaidi wa Basra

14:18 - January 15, 2012
Habari ID: 2256915
Jumuiya ya Maulamaa wa Iraq imelaani vikali mlipuko wa kigaidi uliotekelezwa hapo jana Jumamosi katika umati wa waombolezaji wa Arbaini ya Imam Hussein (as) mjini Basra, ambao ulisababisha vifo vya watu kadhaa na kujeruhi wengine wengi.
Jumuiya hiyo inayoongozwa na Sheikh Khalid al-Mulla kupitia taarifa imelaani hujuma hiyo ya kigaidi iliyotekelezwa katika eneo la az-Zeibar kusini mwa Basra sambamba na kufanyika maombolezo ya Arbaini ya Imam Hussein (as).
Imesema hujuma hiyo ambayo imeitaja kuwa ni jinai ya kutisha, ni katika mfululizo wa ugaidi unaotekelezwa dhidi ya raia wasio na hatia wa Iraq, ugadi ambao unaungwa mkono na baadhi ya serikali zisizokubaliana na serikali ya hivi sasa ya Iraq.
Jumuiya ya Maulamaa wa Iraq pia imelaani fitina zinazoenezwa na baadhi ya wanasiasa na wabunge wa nchi hiyo na kusisitiza kwamba jambo hilo ni sawa na kuunga mkono ugaidi dhidi ya wananchi wa nchi hiyo.
Jumuiya iliyotajwa imewataka wanazuoni wa ndani na nje ya Iraq kufanya juhudi maradufu kwa lengo la kupambana na mielekeo ya kupindukia mipaka iliyoko miongoni mwa Wairaki na kuhubiri ujumbe wa kuvumiliana na kuishi pamoja kwa amani wananchi wote wa nchi hiyo.
Vyombo vya hospitali vya mjini Basra vimetangaza kwamba watu 53 waliuawa shahidi na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi. Ripoti zinasema kuwa, shambulio hilo la kinyama dhidi ya waombolezaji lilitekelezwa na gaidi wa kike aliyekuwa amevalia mavazi ya polisi katika kituo kimoja cha upekuzi katika mji wa Basra. 934981
captcha