Kikao cha kwanza cha Bunge la Misri kinafanyika leo ikiwa zimebakia siku mbili tu kabla ya maadhimisho ya kwanza ya kuanza harakati za mapinduzi ya Misri Januari 25 mwaka jana, harakati ambazo zilifikia kilele Februari 11 baada ya dikteta Hosni Mubarak kulazimika kujiuzulu.
Chama cha Uhuru na Uadilifu (FJP) ambacho ni tawi la kisiasa la Ikhwanul Muslimini nchini Misri kimeshinda viti 235 vya Bunge, sawa na asilimia 47.18 ya kura zilizopigwa katika duru zote tatu za uchaguzi wa Bunge.
Katika kikao cha leo, Bunge la Misri linatarajiwa kumchagua Muhammaed al-Katatni kuwa Spika wa kwanza wa Bunge la nchi hiyo baada ya kuangushwa utawala wa Hosni Mubarak. Aidha Bunge hilo linatarajiwa kuteua kamati ya watu 100 itakayokuwa na jukumu la kuandaa katiba mpya.
Kwa vile wanaharakati wa Kiislamu sasa wanaongoza bunge la Misri, ni jambo lisilo na shaka hata kidogo kwamba watapata ushindi mkubwa pia katika uchaguzi wa Baraza la Shura. Hata hivyo madola ya kigeni ambayo hayakufurahishwa hata kidogo na mabadiliko yaliyotokea huko Misri hasa kupata nguvu wanaharakati wa Kiislamu, tayari wanaeneza uvumi kuwa wanaharakati hao wanataka kuhodhi madaraka yote nchini Misri. Wakati ambapo Ikhwanul Muslimin wameshasema tangu zamani kuwa wataunda serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayoshirikisha matabaka yote ya wananchi wa Misri. Tab'an wamesisitiza pia kuwa lengo lao kuu ni kuirejeshea Misri heshima yake ya Kiislamu kwani wanaamini kuwa Uislamu ndiyo njia pekee ya wokovu wa mwanadamu duniani na Akhera.
939700