Kwa mnasaba wa kuwadia mwezi wa Rabiul Awwal ambamo alizaliwa Bwana Mtume SAW, Waislamu nchini Albania wameandaa kongamano lenye anwani ya 'Muhammad SAW, Kigezo Bora Zaidi kwa Wanadamu' katika mji mkuu, Tirana.
Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA barani Ulaya, kongamano hilo lilifanyika Februari tatu na lilitayarishwa na Kamati ya Waislamu wa Albania. Watu wa matabaka mbalimbali ya jamii walishiriki katika kongamano hilo.
Hotuba kuhusu sira ya Mtume SAW na makala kuhusu 'Shakhsia ya Kimataifa ya Mtume SAW' na 'Maadili ya Mtume SAW' ziliwasilishwa katika kongamano hilo na Ali Zaeemi na Nasif Huja kwa taratibu.
Baada ya kumalizika kikao hicho washiriki walitunukiwa kitabu kilichokuwa na anwani ya 'Sira ya Mtume SAW' pamoja na vitabu vingine kuhusu Hadhiti za Mtume SAW na masuala ya Kiislamu.
Waislamu kote duniani wanaadhimisha sherehe za Miladun Nabii katika mwezi huu wa Rabiul Awwal-Mfunguo Sita. Mbali na sherehe hizo pia kunafanyika Wiki ya Umoja kati ya tarehe 12-17Rabiul Awwal.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa kuhusiana na kuzaliwa Bwana Mtume SAW kuna riwaya mbili mashuhuri. Waislamu wengi wa madhehebu ya Kisuni wanaamini kwamba, Bwana Mtume SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka wa tembo uliosadifiana na mwaka 570 Miladia.
Kundi jengine la Waislamu ambalo linaundwa zaidi na Waislamu wa madhehebu ya Kishia linaamini kwamba, Mtume wa Uislamu alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka huo huo. Mitazamo hiyo miwili takribani pengo lake ni kipindi cha wiki moja. Kwa kuzingatia hali hiyo, Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini (MA) Mwasisi na Mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikitangaza kipindi hiki cha wiki moja kuwa Wiki ya Umoja, ili Waislamu badala ya kuvutana na kuanza kukuza tofauti za tarehe za kuzaliwa Bwana Mtume SAW wakae pamoja na kujadili umuhimu wa umoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili Waislamu na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla.
945447