IQNA

Wanazuoni wa Kishia wa Saudia wakemea mauaji ya waandamanaji

15:54 - February 13, 2012
Habari ID: 2273214
Wanazuoni wa Kishia wa Saudi Arabia wamekemea vikali ufyatuaji risasi wa moja kwa moja unaofanywa na askari wa nchi hiyo dhidi ya waandamanaji ambao hivi karibuni umepelekea kuuawa vijana wawili katika eneo la wakazi wengi wa Kishia la as-Sharqiya.
Akizungumzia suala hilo Muhammad al-Habib mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Saudia katika mji wa Safawi amesema kuwa mauji yaliyofanywa hivi karibuni dhidi ya vijana hao waliokuwa wakipigania haki zao za msingi kwa njia ya amani ni mbinu inayotumiwa na utawa dhalimu wa Saudia ambao haufahamu lugha nyingine isipokuwa ya mabavu na ukandamizaji dhidi ya wananchi wake.
Amesema ukandamizaji huo hautakuwa na faida yoyote kwa utawala huo na kusisitiza kuwa njia pekee ya kumaliza malalamiko ya wananchi ni kuwarejeshea haki zao zote za kimsingi ambazo zinatambuliwa kote duniani.
Katika upande wa pili Ayatullah Namr an-Namr Imam wa Swala ya Ijumaa ya mji wa Awamiyya amewahutubu vijana wa nchi hiyo kwa kusema kuwa kujibu silaha kwa silaha ni takwa linalofuatiliwa na utawala wa Saudia na amewataka wajiepushe na jambo hilo. Amesema wanatakiwa kufuatilia malengo yao kwa kujiepusha na vitendo vya ghasia, kujieleza bila woga na kwa kutegemea imani.
Ayatullah Namr amekadhibisha madai ya watawala wa nchi hiyo kwamba milango ya ukosolewaji serikali iko wazi na kusisitiza kuwa milango iliyo wazi kwa wapinzani ni ya jela.
Akijadili suala hilohilo, Munir al-Khabbaz mwanazuoni mwingine mashuhuri wa Saudia amesema kuwa kwa mtazamo wa dini tukufu ya Kiislamu kulindwa heshima ya muumini ni muhimu zaidi kuliko kulindwa heshima ya al-Kaaba lakini kwamba siasa zinazotekelezwa na utawala wa Saudia unaotumia ovyo silaha dhidi ya raia wake ni kinyume kabisa na mafundisho hayo muhimu ya Kiislamu.
Wakati huohuo, Sheikh Abdul Karim al-Habil, mwanazuoni mwingine wa Saudia amesema kwamba inasikitisha kuona kwamba utawala wa Riyadh unatumia nguvu na mabavu dhidi ya waandamanaji wanaoandamana kwa amani badala ya kusikiliza kwa makini matakwa yao.
Mashia wa Saudia siku za Alkhamisi na Ijumaa iliyopita walifanya maandamano makubwa dhidi ya utawala wa Riyadh ambapo vijana wawili waandamanaji walilengwa na kuuawa kwa risasi za moja kwa moja na askari wa utawala huo. 951843
captcha