Sheikh Muhammad Hussein ametoa taarifa akisema kwamba ni jambo la kushangaza na kuchekesha kuona kwamba utawala haramu wa Israel ambao unadai kutetea demokrasia unawakandamiza Wapalestina na kutoruhusu adhana katika misikiti yao.
Mufti huyo wa Quds na Palestina amesisitiza kwamba Wapalestina wanaheshimu na kutetea sheria zote zinazounga mkono uhuru wa ibada. Ametahadharisha dhidi ya vitendo vya kuvunjia heshima misikiti ambayo ni sehemu muhimu ya ibada na kuongeza kuwa huenda jambo hilo likachochea vita vya kidini katika siku zijazo. Amezitaka nchi za Kiislamu na Kiarabu na vilevile jamii ya kimataifa kuchukua hatua za dharura kwa lengo la kusimamisha mara moja uvunjiwaji heshima misikiti ya Palestina na hasa Msikiti wa al-Aqsa.
Katika hatua ya ubaguzi wa rangi, utawala haramu wa Israel umefuta majina ya Haram ya Nabii Ibrahim mjini al-Khalil na Msikiti wa Bilal bin Rabah huko Palestina katika orodha ya maeneo ya kale kitaifa yanayopasa kuhifadhiwa na kutengewa bajeti.
Mahakama Kuu ya utawala wa Tel Aviv siku ya Alkhamis Jumatatu ilitoa hukumu ya kupiga marufuku adhana katika Msikiti wa Burin mjini Nablos na pia kutaka taa za msikiti huo zizimwe. Hukumu hiyo imetolewa wakati ambao Waislamu wa eneo hilo walikuwa wakijitayarisha kuswali swala ya kwanza ya jamaa katika msikiti huo baada ya kukamilika ujenzi wake. 954270