Kwa mujibu wa taarifa, asilimia 65 ya wapiga kura miliono 48 kote Iran wameshiriki katika uchaguzi wa kuwachagua wabunge 290.
Kwa kushiriki kwa wingi katika zoezi hilo la kisiasa wananchi wa Iran kwa mara nyingine tena wamethibitisha nafasi yao muhimu katika maamuzi ya nchi na uungaji mkono wao kwa mfumo wa Kiislamu. Umati mkubwa wa wananchi katika pembe zote za nchi ulifika mapemba kwenye vituo tofauti vya kupigia kura, hata kabla ya kufunguliwa vituo hivyo, ili kupata fursa ya kuwachagua wawakilishi wao bungeni.
Tokea saa mbili asubuhi leo Ijumaa wananchi wamekuwa na masaa 10 ya kushiriki katika zoezi hilo muhimu la kitaifa la upigaji kura ili mbali na kuainisha mustakbali wao wenyewe, waweze pia kuwathibitishia walimwengu itibari na nguvu kubwa ya mfumo wa Kiislamu wa Iran. Muda huo umerefushwa katika baadhi ya vituo vya upigaji kura nchini ili kuwawezesha wananchi waliofika kwa wingi na kwa hamu kubwa katika vituo hivyo, kuweza kushiriki katika zoezi hilo la kitaifa. Ni wazi kuwa kila mara idadi ya wananchi wanaoshiriki katika uchaguzi mkuu inavyokuwa kubwa ndivyo mfumo wa Kiislamu wa Iran inavyopata itibari na nguvu kubwa zaidi ya kuweza kukabiliana na njama za maadui wake. Kwa kuzingatia umuhimu wa jambo hilo, sambamba na mahudhurio makubwa ya wananchi katika vituo vya kupigia kura za uchaguzi wa Bunge la Tisa la Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, viongozi wa ngazi za juu wa Mfumo wa Kiislamu na wanazuoni mashuhuri wa kidini pia wamefika mapema kwenye vituo vya kupigia kura ili kuwachagua wabunge wanaoona kwamba wanafaa kuwakilisha wananchi kwenye shughuli za bunge. Viongozi na wanazuoni hao waliongozwa na Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyefika kwenye kituo cha kupigia kura mapema asubuhi ili kushiriki kwenye zoezi muhimu la kidini na kisiasa la kuteuliwa wabunge wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Akizungumza mbele ya waandishi habari mara tu baada ya kupiga kura, Ayatullah Khamenei amesema kuwa uchaguzi wa mara hii una umuhimu mkubwa kwa kuzingatia masuala yanayojiri sasa ulimwenguni. Amesisitiza kwamba licha ya kuwa uchaguzi nchini Iran huthibitisha ukweli wa mambo yanayojiri nchini, lakini pia una ujumbe maalumu kwa waungaji mkono na maadui wa mfumo wa Kiislamu kwa wakati mmoja. Amesema azma thabiti ya taifa la Iran katika kipindi cha miaka 33 iliyopita ni jambo lenye umuhimu mkubwa. Ameongeza kuwa katika mapinduzi mengine duniani wananchi huonyesha kuchoshwa na mapinduzi waliyofanya na kufuata njia tofauti na ile waliyoainisha mwanzoni, lakini kwamba hali ni tofauti kabisa kuhusiana na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Amesema uchaguzi wa leo umefikisha ujumbe huu kwa walimwengu kwamba licha ya kupita miaka 33 ya mapinduzi lakini wananchi wangali wanaunga mkono na kuwa na imani kubwa na mfumo huu ambao wamesimama imara kutetea malengo yake matukufu.
Naye Ayatullah Hashimi Rafsanjani, Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu amewaambia waandishi habari mara tu baada ya kupiga kura kwamba umoja na mshikamano wa taifa la Iran una umuhimu mkubwa hasa kwa kutilia maanani matukio muhimu yanayojiri sasa katika Mashariki ya Kati. Viongozi na wanazuoni wengine mashuhuri walioshiriki kwenye uchaguzi wa leo wakiwemo Marja' taklidi Ayatullah Nassir Makarim Shirazi na Hussein Nuri Hamedani wamesema kwamba mahudhurio makubwa ya wananchi katika uchaguzi huu, mbali na kuwa ni jukumu la kidini na kimaadili, yana umuhimu mkubwa kwa kuzingatia kuwa yatavunja njama za maadui ambao wamekuwa wakifanya njama za kuuangusha mfumo wa Kiislamu.
Kufuatia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, wananchi wa Iran kwa wastani wamekuwa wakishiriki katika uchaguzi kila mwaka kwa lengo la kuwa na nafasi katika maamuzi ya serikali na kuimarisha mfumo wao wa Kiislamu. Kushiriki kwa wingi na shauku kubwa wananchi wa Iran katika awamu ya tisa ya uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran kunathibitisha wazi mwamko na utambuzi wao wa njama zinazofanywa na maadui dhidi ya mfumo wao wa Kiislamu.
963716