IQNA

Iran yalaani msimamo wa Uingereza kuhusu uchaguzi nchini

11:48 - March 04, 2012
Habari ID: 2285094
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza aliyedai kuwa uchaguzi wa bunge Iran haukuwa 'huru na wa haki'.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Ramin Mehmanparast amesema madai hayo hayana msingi wowote na yanaashiria sera za Uingereza za kuingilia mambo ya ndani ya Iran. Amemtuhumu Hague kuwa alijaribu kudunisha mahudhurio makubwa ya Wairani katika uchaguzi huru na wa haki wa bunge uliofanyika Machi pili.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia amewanasihi watawala wa Uingereza kuheshimu chaguo la taifa la Iran. Siku ya Ijumaa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza alilaani uchaguzi uliofanyika Iran na kudai eti haukuwa wa kidemokrasia. Hii ni katika hali ambayo karibu asilimia 65 ya wapiga kura walishiriki katika uchaguzi huo.
Zaidi ya Wairani milioni 48 walikuwa wametimiza masharti ya kupiga kura katika uchaguzi huo wa juzi.
Matokeo ya awali ya uchaguzi huo yanaonyesha Harakati ya Muungano wa Wanaofungamana na Misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu wamepata ushindi mkubwa. Uchaguzi huo ulikuwa na wagombea 3,444 waliokuwa wakiwania viti 290 bungeni.

Kwa hakika ushiriki mkubwa na wa hamasa wa wananchi katika uchaguzi huo kwa mara nyingine tena unabainisha wazi nguvu ya mfumo wa Kiislamu katika kukabiliana na vitisho pamoja na vikwazo vya maadui. Ushiriki huo unatoa ujumbe wa wazi kwa maadui kwamba hawatafua dafu katika kukabiliana na irada thabiti ya taifa shupavu la Iran. Ukweli wa mambo ni kuwa kadiri wananchi wanavyoshiriki kwa wingi katika uchaguzi ndivyo mfumo wa Kiislamu unavyopata nguvu na uwezo zaidi, na kwa hakika hiyo ndiyo siri ya kuendelea kuimarika mfumo huu katika nyanja zote za kisiasa, kijamii, kiuchumi na kielimu.
Ni wazi kuwa ushiriki mkubwa wa wananchi katika uchaguzi ni jambo linalovunja njama na vitisho vya maadui ambao wanataka kudhoofisha irada ya taifa la Iran. Kwa maelezo hayo ni wazi kuwa maadui wa mfumo wa Kiislamu ambao daima hufanya njama dhidi ya mfumo huu, wametambua vyema kwamba njama zao hizo hushindwa mara kwa mara kutokana na uungaji mkono mkubwa wa wananchi kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa hivyo muda mfupi kabla ya kufanyika uchaguzi wa Ijumaa, vyombo vya habari na kipropaganda vya Magharibi vilifanya juhudi maradufu kwa ajili ya kuchochea na kuwashawishi wananchi wa Iran wasishiriki katika uchaguzi huo. Licha ya kuwa njama kama hizo zilifeli katika chaguzi zilizopita lakini nchi hizo mara hii zilidhani zingefanikiwa kufikia malengo yao kutokana na mambo kadhaa. Jambo la kwanza ni kutumiwa vikwazo na tishio la vita kama chombo cha kuwatisha Wairani wasishiriki kwenye uchaguzi. Licha ya viongozi wa nchi za Magharibi kuendesha propaganda hiyo kubwa dhidi ya Iran lakini walipigwa na butwaa baada ya kuona kwamba wananchi wa Iran hawakushtuliwa na vitisho hivyo bali walijitokeza kwa wingi na kushiriki kwa hamasa katika uchaguzi huo wa kuainisha hatima ya nchi yao mbele ya hujuma ya maadui. Kwa mahudhurio yao makubwa wananchi wa Iran kwa mara nyingine tena wamekariri uzoefu wao wa miaka 33 iliyopita kwa kubatilisha dhana mbaya ya viongozi na vyombo vya habari vya Magharibi kuhusiana na taifa la Iran.

964921
captcha