IQNA

Sayyed Nasrullah: Mapambano yataendelea hadi kukombolewa Quds

13:13 - March 05, 2012
Habari ID: 2285900
Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah cha Lebanon amesema kuwa harakti ya muqawama au mapambano ya nchi hiyo yataendelea hadi kukombolewa Quds Tukufu.
Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa chama cha Hizbullah cha Lebanon amesema kuwa harakti ya muqawama ya nchi hiyo itaendelea hadi kukombolewa Quds Tukufu. Sayyid Nasrullah amesema chama cha Hizbullah kitapambana na mipango na njama za kila leo za maadui zenye lengo la kupoteza utambulisho wa Palestina hususan wa mji wa Quds. Sayyid Hassan Nasrullah ameyasema hayo katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu Quds Tukufu huko Beirut mji mkuu wa Lebanon.
Amesema Hizbullah itasimama imara dhidi ya njama za Israel za kutaka kuiyahudisha Quds Tukufu na kupoteza utambulisho wa kidini wa mji huo mtakatifu. Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amewatolea mwito wafuasi wa dini zote za Mwenyezi Mungu kuchukua hatua za dhati kuhusu mustakbali wa Quds.
Eneo la Quds Mashariki lilidhibitiwa na kukaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel mwaka 1967 na mwaka huo huo Bunge la Israel likaitangaza Quds kuwa ni sehemu ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu. Hii ni katika hali ambayo mwaka 1948, eneo la magharibi mwa Quds lilikaliwa kwa mabavu na jeshi la Israel na tangu awali Wazayuni wakawa wameanzisha mikakati ya kufuta athari na nembo za Wapalestina katika maeneo hayo na kutaka kuyaonyesha kuwa ni ya Kiyahudi. Ukweli wa mambo ni kuwa, tangu mwanzo baada tu ya kukaliwa kwa mabavu Quds Mashariki, viongozi wa Tel Aviv walianza kutekeleza miradi ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Baytul Muqaddas wakiwa na lengo la kubadilisha muundo wa kijamii na kijiografia wa mji huo mtakatifu. Mwaka 2002 Israel ilitekeleza mpango wa ujenzi wa ukuta wa kibaguzi na kupora sehemu ya ardhi za Quds kwa kisingizio cha kujenga ukuta huo. Kwa muktadha huo, mbali na kupora ardhi za Wapalestina ikawa imefanya mzingiro dhidi ya Quds Tukufu. Hii ni katika hali ambayo, mnamo mwaka 1993 utawala huo ghasibu ulikuwa umeahidi katika hati ya makubaliano ya Oslo juu ya kusitisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Quds Mashariki na badala yake kutatua kadhia ya mji huo kupitia njia ya mazungumzo na Wapalestina. Katika mazingira kama hayo na katika kujibu siasa za uharibifu na za kujitanua za Israel, Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah amesisitiza kuwa, Quds haiwezi kukombolewa kupitia njia ya mazungumzo na Wazayuni na kwamba, chaguo la mazungumzo na maghasibu hao halina faida yoyote ile.
965240
captcha