IQNA

Hamas yalaani kutiwa nguvuni tena mateka walioachiliwa huru hivi karibuni

16:26 - March 05, 2012
Habari ID: 2286114
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imelaani vikali hatua ya utawala haramu wa Israel ya kuwatia nguvuni tena mateka wa Kipalestina uliowaachilia huru hivi karibuni mkabala na kuachiliwa huru askari mmoja wa utawala huo aliyetekwa nyara na harakati hiyo ya Kiislamu.
Hamas imesema kuwa utawala haramu wa Israel umetekeleza hatua hiyo inayokwenda kinyume na sheria za kimataifa pamoja na mapatano ya pande mbili kwa lengo la kudhoofisha motisha ya wafungwa wa Palestina wanaoteseka katika jela za kuogofya za utawala huo. Utawala wa Kizayuni umemtia nguvuni tena Hanna Shalbi, mwanamke mateka wa Kipalestina aliyeachiliwa huru hivi karibuni kutoka kwenye jela za utawala huo. Mwanamke huyo amekuwa akisusia chakula kulalamikia hatua hiyo ya kidhulma ya Israel. Hamas imeitaka Misri ambayo imekuwa ikisimamia suala la mabadilishano ya mateka wa Palestina wanaozuiliwa katika jela za Israel pamoja na makundi ya kutetea haki za binadamu kuingilia kati suala hilo na kutoa mashinikizo dhidi ya utawala wa Tel Aviv ili umwachie huru mara moja mwanamke huyo na wafungwa wengine wa Palestina wanaoendelea kuteseka katika jela za utawala huo. Ripoti nyingine zinasema kuwa utawala wa Israel katika kipindi cha miezi michache iliyopita umewakamata tena Wapalestina wengine watano walioachiliwa huru hivi karibuni na utawala huo, ambao walikuwa miongoni mwa mateka 350 walioachiliwa huru katika siku za hivi karibuni. 965290
captcha