Wakizungumza mjini Kampala siku ya Ijumaa katika kongamano la kuadhimisha mwaka wa 170 tokea Uislamu uingie Uganda, Waislamu wamesema kinyume na madai ya huko nyuma ya serikali , hivi sasa idadi kubwa ya Waislamu nchini humo wamepata masomo ya juu kabisa na wana uwezo wa kushikilia nafasi muhimu serikalini. Gazeti la Sunday Monitor limemnukulu Dr. Salim Simba Kayuga mhadhiri mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Makerere akisema Museveni anapaswa kuwazingatia Waislamu katika mabadiliko ya baraza la mawaziri. Akizungumza katika kongamano hilo, Dr. Kayuga amewasilisha makala iliyojadili suala la kutengwa Waislamu Uganda ambapo ametoa mfano wa kubaguliwa Waislamu katika Wizara ya Mambo ya Nje Uganda. Amesema Wizara ya Mambo ya Nje ina idara 19 lakini hakuna hata idara moja inayoongozwa na Muislamu. Aidha kati ya wafanyakazi 277 wa ngazi za juu katika wizara hiyo kuna Waislamu 13 tu. Dr. Kayuga amelalamika kuwa Waislamu hupewa zaidi kazi za udereva wizarani humo. Katika ujumbe wake kwa kongamano hilo, Rais Yoweri Museveni amewapongeza Waislamu kwa munasaba wa kutimia mwaka wa 170 tokea Uislamu uingie nchini humo. Amesema kuwa serikali yake itazidi kushirikiana na Waislamu. Kwa mujibu wa Shirika la Utaifti la Pew Forum idadi ya Waislamu Uganda ni milioni nne katika nchi hiyo yenye idadi ya watu takribani milioni 33. Uganda pia ni mwanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu OIC.
965893