Wanachuo wa Kiislamu wa Pakistan jana Jumamosi walifanya maandamano ya kulaani hatua ya askari jeshi wa Marekani ya kuchoma moto kitabu kitakatifu cha Waislamu, Qur'ani, katika kituo chao cha kijeshi huko Bagram nchini Afghanistan.
Kwa mujibu wa gazeti la Pakistan la The News Muungano wa Wanachuo Waislamu wa Pakistan MSF na Muungano wa Wanachuo FTF ilifanya maandamano tofauti huko katika mji wa Peshawar kulaani kitendo hicho cha dharau cha askari wa Marekani dhidi ya matukufu ya Kiislamu. Wanachuo walioshiriki kwenye maandamano hayo walibeba mabango yaliyokuwa na nara za kulaani Marekani na washirika wao nchini Afghanistan.
Viongozi wa miungano hiyo miwili ya wanachuo walizungumza katika hadhara ya waandamanaji na kusisitiza kwamba kuvunjiwa heshima kitabu kitakatifu cha Qur'ani ni jambo lisiloweza kuvumiliwa na Waislamu na kwamba askari wa Marekani wamewakasirisha sana Waislamu kutokana na kitendo chao cha kuchoma moto Qur'ani.
Waandamanaji wametaka kuadhibiwa wahusika wote wa kitendo hicho cha dharau dhidi ya matukufu ya kidini na kuitaka serikali ya Islamabad kutizama upya uhusiano wake na utawala wa Washington. 969429