IQNA

Kiongozi wa Ansarullah: Watu wa Yemen wameinua bendera ya Jihadi dhidi ya mabeberu wa zama

22:13 - September 04, 2025
Habari ID: 3481183
IQNA-Kiongozi wa harakati ya Ansarullah, Sayyid Abdulmalik Badruddin al-Houthi, amesisitiza kuwa watu wa Yemen wanaendelea kufuata mwenendo wa Mtume Muhammad (S.A.W) na mafundisho ya Qur’an Tukufu.

Amesema kuwa watu wa Yemen wameinua bendera ya jihadi dhidi ya mabeberu wa zama hizi, ubeberu wa Kizayuni wa kimataifa, na wale wanaounga mkono uovu huo kama vile Marekani.

Kwa mujibu wa ripoti ya Al-Masirah iliyonukuliwa na IQNA, al-Houthi alizungumza mapema leo Alhamisi katika maadhimisho ya Maulidi ya Mtume Muhammad (SAW), akieleza kuwa sherehe hizo ni za kipekee nchini Yemen na ni ishara ya imani ya watu wake. Alitaja siku hiyo kuwa ni fursa ya kushukuru, kuimarisha imani, na kufanya mema.

 Katika hotuba yake, al-Houthi alikemea mashambulizi ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza yanayoungwa mkono na Marekani, akiyataja kuwa ni “jinai ya karne na fedheha ya waliopuuza wajibu wao.” Aliongeza kuwa mateso ya watu wa Palestina yamefikia kiwango cha kutisha, kiasi kwamba hata maziwa ya watoto yananyimwa, huku adui wa Kizayuni akiendelea kuvamia Msikiti wa Al-Aqsa na Ukingo wa Magharibi kila siku.

Yemen Imejizatiti kwa Jihadi Dhidi ya Mabeberu wa Zama

Sayyid  Badruddin al-Houthi amesisitiza kuwa mpango wa utawala wa Kizayuni hauishii Palestina pekee, bali unalenga kubadilisha ramani ya Mashariki ya Kati na kuunda "Israeli Kubwa". Amesema kuwa njia zote mbadala ambazo Umma wa Kiislamu umejaribu zimefeli, na ni nuru ya Mwenyezi Mungu pekee inayoweza kumkomboa binadamu kutoka kwenye ujinga wa zama.

Ukandamizaji wa Kizayuni na Mshirika Wake Marekani

Sayyid  Badruddin al-Houthi amelaani vikali mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza, akisema yanatekelezwa kwa msaada wa Marekani na mataifa ya Magharibi. Amesema mamilioni ya watu, wakiwemo watoto na wazee, wanakumbwa na njaa, huku mashambulizi hayo yakifanywa kwa silaha za kisasa. Idadi ya mashahidi, majeruhi na waliopotea imefikia zaidi ya 230,000 katika kipindi cha siku 690. 

Kuvunjwa kwa Heshima ya Msikiti wa Al-Aqsa

Ameeleza kuwa uvunjaji wa heshima ya Msikiti Mtukufu wa Al-Aqsa  jijini Al Quds (Jerusalem) unatekelezwa na Waisraeli  kila siku, na kuna vitisho vya kuuharibu. Waisraeli wanajaribu kuzuia Wapalestina kurudi katika ardhi yao, huku baadhi ya nchi za Kiislamu zikikaa kimya au kushirikiana na adui.

Hatari ya Vita Baridi na Kushuka kwa Maadili ya Umma

Sayyid  Badruddin al-Houthi ameonya kuhusu vita baridi vinavyoendeshwa na Wazayuni dhidi ya Waislamu bilioni mbili, akisema vinawalazimisha kuwa wanyonge na kujisalimisha. Ameeleza kuwa baadhi ya tawala za Kiarabu na Kiislamu zimekosa msimamo, hali inayochochea  utawala wa Kizayuni upate kiburi cha kuendeleza jinai zake.

Wito wa Kurudi kwa Qur’an na Mtume Muhammad (S.A.W)

Amesisitiza kuwa njia pekee ya wokovu ni kushikamana na Qur’an na mwenendo wa Mtume Muhammad (SAW). Ameeleza kuwa Mtume alizaliwa Makkah mwaka wa "Amul-Fil", na akalelewa kwa ulinzi wa Mwenyezi Mungu kupitia babu yake na ami yake Abu Talib. Mtume alikuwa na maadili bora, hekima na uaminifu wa hali ya juu.

Mapambano ya Mtume Dhidi ya Washirikina na Wazayuni

Sayyid  Badruddin al-Houthi  amekumbusha kuwa Mtume Muhammad (SAW) aliongoza mapambano dhidi ya washirikina, Wayahudi na Warumi, akiwafundisha Waislamu kuwa na msimamo thabiti. Vita vya Banu Qaynuqa, Banu Qurayza na Khaybar vilikuwa pigo kwa Wayahudi, na ushindi wa Makkah ulileta mwamko wa Kiislamu katika eneo lote.

Wito kwa Umma wa Kiislamu na Watu wa Kitabu

Amehimiza Waislamu na watu wa Kitabu  kujibu wito wa Mwenyezi Mungu, kuabudu Mola Mmoja na kukataa ushirikina. Amesema kuwa Umma wa Kiislamu unapaswa kuonyesha mapenzi ya kweli kwa Mtume Muhammad (SAW) kwa vitendo, si maneno tu.

Kujitolea kwa Yemen kwa Jihadi na Palestina

Hatimaye, Sayyid Badruddin al-Houthi  amepongeza msimamo wa watu wa Yemen katika kuendeleza jihadi dhidi ya mabeberu wa zama, akisisitiza kuwa wataendelea kushikilia bendera ya mapambano hadi ushindi upatikane. Ameomba msaada wa Mwenyezi Mungu kwa watu wa Palestina na ushindi kwa haki.

4303379

 

 

Habari zinazohusiana
captcha