IQNA

Kikao cha kimataifa cha muujiza wa Qur'ani na Suna za Mtume (saw) chaanza Cairo

14:33 - March 14, 2012
Habari ID: 2291606
Kikao cha sita cha kimataifa ambacho hufanyika kila mwaka kuhusiana na muujiza wa kielimu wa Qur'ani Tukufu na Suna za Mtume (saw) kilianza jana Jumanne katika chuo cha ufundi cha al-Mansuriyya huko mjini Cairo Misri.
Kikao hicho kimedhaminiwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Muujiza wa Kielimu wa Qur'ani na Suna za Mtume (saw) na kwa ushirikiano wa uongozi wa Chuo Kikuu cha al-Mansura.
Kikao hicho ambacho kilianza jana na kuhudhuriwa na Sayyid Abdul Khaliq, mkuu wa chuo kilichotajwa na Abdullah al-Muslih, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimtaifa ya Muujiza wa Kielimu wa Qur'ani na Suna za Mtume (saw) kitamalizika kesho al-Khamisi.
Wasomi na shakhsia waliopangiwa kuzungumza katika kikao hicho ni pamoja na Ahmad Hijazi, mhadhiri wa Kituo cha Kitaifa cha Utafiti cha Misri, Muhammad Imam Dawoud Mkuu wa Taasisi ya Walimu wa Qur'ani ya Cairo, Yahya Waziri, mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Uhubiri wa Kiislamu na Abdul Jawad as-Swawi, Mshauri wa Masuala ya Kielimu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Muujiza wa Kielimu wa Qur'ani na Suna za Mtume (saw).
Akizungumzia kikao hicho, Jeihan Fuad Mkuu wa Kituo cha Upashaji Habari cha Chuo Kikuu cha al-Mansuriyya amesema kwamba ni fahari kubwa kwa chuo hicho kuandaa kikao hicho muhimu ambacho kinawashirikisha wasomi pamoja na wanafikra muhimu wa ulimwengu wa Kiislamu. Ameongeza kwamba Jumuiya ya Kimataifa ya Muujiza wa Kielimu wa Qur'ani na Suna za Mtume (saw) imefanya juhudi kubwa za kubainisha muujiza wa kielimu wa kitabu kitakatifu cha Qur'ani na Suna za Mtume duniani. 971814
captcha