Sayyid Hassan Nasrullah aliyasema hayo juzi Ijumaa katika hotuba aliyotoa huko Dhahiyah kusini mwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut kwa mnasaba wa kuadhimisha Siku ya Ardhi. Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema kama ninavyomnukuu:" Siku hii ni katika siku za Palestina na miongoni mwa siku za Quds; na katika siku hii ndugu zetu wa Palestina walioko ndani na wale walioko nje ya Palestina wanaandamana ili kuonesha mshikamano wao", mwisho wa kumnukuu.
Katibu Mkuu wa Hizbullah ameongeza kuwa wavamizi na wale wanaoshirikiana nao wanataka wananchi wa Palestina na umma wa Kiislamu waisahau Palestina, lakini kutokana na sababu nyingi wameshindwa kulitoa suala la Palestina nje ya mduara wa masuala muhimu. Sayyid Hassan Nasrullah amesisitiza kuwa muqawama ndio sababu iliyoifanya kadhia ya Palestina iendelee kubaki hai hadi hii leo, na njama zote zilizofanywa kwa kutumia mamia ya mabilioni ya dola ili kuizima na kuifuta kadhia hiyo zimegonga mwamba.
Kutokana na msimamo dhaifu wa jamii ya kimataifa na jumuiya za kieneo hususan Ulimwengu wa Kiarabu, utawala wa Kizayuni ungali unaendeleza siasa zake za kujitanua. Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilitangaza hapo kabla kuwa kuunga mkono kivitendo suala la Palestina itakuwa moja ya ajenda kuu za kikao cha 23 cha jumuiya hiyo kilichofanyika mjini Baghdad. Hata hivyo licha ya umuhimu liliopewa suala hilo, katika kikao cha Baghdad kama ilivyokuwa katika vikao vya kabla yake baadhi ya nchi za Kiarabu zinazounga mkono kufanya mapatano na utawala wa Kizayuni zilikwamisha upitishaji maamuzi ya maana na ya kivitendo ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina.
Alaa kulli haal hii si mara ya kwanza kutolewa kauli na kuchukuliwa misimamo ya kuunga mkono kufanya mapatano na utawala wa Kizayuni katika vikao vya viongozi wa Arab League, bali kimsingi hasa ni kwamba katika vikao vingi vya Jumuiya hiyo ya Waarabu vilivyofanyika katika miongo miwili iliyopita limekuwa likitolewa sisitizo na kutiliwa mkazo suala la kufanya mapatano na utawala haramu wa Israel. Upeo wa msimamo dhaifu wa nchi za Kiarabu katika kukabiliana na adui Mzayuni na waungaji mkono wake ulionekana katika mpango wa mapatano uliopewa jina la mpango wa amani wa Waarabu uliopendekezwa na viongozi wa Saudi Arabia katika kikao cha mwaka 2002 cha viongozi wa Araba League, mpango ambao umefumbia macho haki nyingi za wananchi madhulumu wa Palestina. Mbali na kufumbia macho kikamilifu suala la wafungwa wa Kipalestina na haki ya wakimbizi wa Kipalestina kurejea katika ardhi zao za asili, mpango huo hautoi hakikisho kamili pia la kupatikana haki nyengine za Wapalestina.
Lakini pamoja na yote hayo sisitizo la wananchi wa Palestina na wa mataifa ya eneo la kuendeleza muqawama dhidi ya Wazayuni limezima njama za utawala ghasibu wa Israel, madola ya Magharibi pamoja na baadhi ya nchi za Kiarabu zenye lengo la kulifuta suala la Palestina; na huo ndio ukweli uliotiliwa mkazo na Katibu Mkuu wa Hizbullah katika hotuba yake aliyotoa kwa mnasaba wa Siku ya Ardhi.../
976539