Al Tibi ameviambia vyombo vya habari kwamba dharau iliyofanywa na kundi hilo dhidi ya Qur'ani na matukufu ya Waislamu ni kielelezo cha kuporomoka, ufisadi wa kiakhlaki na kisiasa na uhasama wao dhidi ya Uislamu.
Ahmad al Tibi amesema kuwa mashtaka dhidi ya wanaharakati wa mrengo wa kulia wa Israel yatawasilishwa rasmi mahakamani katika kipindi cha wiki mbili zijazo baada ya kukusanywa nyaraka na ushahidi wa kutosha.
Awali wanaharakati wenye misimamo mikali wa Kiyahudi walivunjia heshima kitabu kitakatifu cha Qur'ani katika kurasa zao za Facebook na kudai kuwa Qur'ani Tukufu inashabihiana na kitabu cha "Mein Kamph" cha dikteta wa zamani wa Ujerumani Adolph Hitler.
Kundi hilo la Mayahudi lilichapisha matusi hayo katika ukurasa wa Facebook wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Evigdor Lieberman na kurasa za wawakilishi kadhaa wa bunge la utawala huo haramu.
Hii si mara ya kwanza kwa Wayahudi wenye misimamo mikali kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu. Wiki chache zilizopita Wayahudi hao walichoma moto nakala za Qur'ani na misikiti ya Waislamu katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, tukio ambalo limewajeruhi mno Waislamu kote duniani. 980538