Khatibu wa Sala ya Ijumaa wiki hii mjini Tehran Ayatullah Muhammad Imami Kashani amemnukuu Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyesisitiza mara kadhaa kwamba Iran haina haja ya kuwa na silaha za nyuklia, na kusema kwamba shughuli zote za nyuklia za Tehran zinafanyika kwa malengo ya kisayansi na ni za amani kikamilifu.
Sambamba na kuza duru mpya ya mazungumzo kati ya Iran na Kundi la 5+1 huko mjini Istanbul, Uturuki, Ayatullah Imami Kashani amesisitiza kuwa, pande za mazungumzo hayo zinapaswa kuzingatia nguvu, uwezo na maendeleo ya Iran.
Duru mpya ya mazungumzo kati ya Iran na kundi la 5+1 linalowajumuisha wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Ujerumani inafanyika leo Jumamosi nchini Uturuki.
Aidha Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya jana mjini Tehran alitoa mkono wa pongezi kwa mnasaba wa kukaribia siku ya jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tarehe 17 Aprili na kusema kuwa, vikosi vya jeshi la Iran siku zote vimekuwa na nafasi muhimu na endelevu katika kuimarisha usalama wa eneo la Ghuba ya Uajemi na kulinda ardhi yote ya taifa hili.