IQNA

Pentagon yasimamisha masomo yanayoupinga Uislamu katika chuo cha jeshi la Marekani

19:15 - April 28, 2012
Habari ID: 2313686
Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon imesimamisha masomo dhidi ya Uislamu yaliyokuwa yakitolewa katika chuo cha kijeshi cha mji wa Norfolk katika jimbo la Virginia baada ya mwanafunzi mmoja kuwasilisha mashtaka kuwa masomo hayo yanapiga vita dini ya Uislamu.
Tovuti ya Islam Today imeripoti kuwa chuo hicho cha mafunzo ya kijeshi ambacho kilikuwa kikitoa mafunzo chini ya anwani ya "Mitazamo katika Uislamu Uislamu na Misimamo Mikali ya Kiislamu", kilikuwa kikitoa masomo yanayopiga vita Uislamu kwa wanafunzi wake ambayo sasa yamesimamishwa baada ya mashtaka hayo.
Masomo hayo yamesimamishwa kwa shabaha ya kuanza uchunguzi juu ya jinsi yalivyoanzishwa na jinsi yalivyokuwa yakitayarishwa na kufikishwa chuoni hapo.
Moja ya mambo yaliyokuwa yakifundishwa kwa wanafunzi wa chuo hicho cha jeshi la Marekani ni somo lenye anwani ya "Marekani katika Vita na Uislamu."
Kashfa hiyo imemlazimisha kamanda wa majeshi yote ya Marekani Jenerali Martin E. Dempsey atoe amri ya kuchunguzwa masomo yote yanayotolewa kwa wananeshi wa nchi hiyo na kuhakikisha kwamba hayatakuwa tena na masomo kama hayo.
Mashtaka dhidi ya masomo hayo yanayopiga vita Uislamu katika jeshi la Marekani yaliwasilishwa Pentagon jana na muda mfupi baadaye ilianzisha uchunguzi kuhusu suala hilo. 994993

captcha