IQNA

Wabahraini waendeleza maandamano kupinga utawala wa Aali Khalifa

17:07 - April 29, 2012
Habari ID: 2314314
Maelfu ya Wabahraini wameendelea kufanya maandamano ya amani katika pembe mbalimbali za nchi hiyo dhidi ya utawala wa Aali Khalifa.
Huku wakipiga nara za kulaani jinai zinazotekelezwa na utawala huo na kutaka uondoke madarakani, waandamanaji wametaka askari wote wa kigeni na hasa wa Saudi Arabia wanaousaidia utawala huo kukandamiza raia wa Bahrain, waondoke mara moja katika ardhi ya nchi hiyo. Wametaka pia kuachiliwa huru wafungwa wote wa kisiasa wanaoteseka katika jela za utawala huo, na hasa Abdul Hadi al-Khawaj, ambaye anaendelea kususia chakula gerezani.
Awali Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International, lilikuwa limetoa taarifa likitaka Abdul Hadi al-Khawaj aachiliwe huru mra moja. Ripoti zinasema kwamba siku ya Alkhamisi maelfu ya Wabahraini walishiriki katika mazishi ya Swalah Abbas mwanamapinduzi ambaye aliuawa hivi karibuni kwa kupigwa risasi na askari usalama wa utawala wa Aali Khalifa. Mazishi hayo baadaye yaligeuka na kuwa maandamano makubwa dhidi ya uatawala huo unaotumia askari wa Saudia kukandamiza raia wa Bahrain wanaopigania haki zao kwa njia za amani. Washiriki wa maandamano hayo walipiga nara za kutaka kung'olewa madarakani utawala wa Mfalme Hamad bin Isa Aali Khalifa na kusisitiza kwamba wako tayari kuendelea kutoa roho zao kwa lengo la kuleta uhuru na uadilifu nchini humo. Kufuatia maandamano hayo askari usalama walitumia gesi ya kutoa machozi na kuwafyatulia risasi waandamanaji ambapo makumi miongoni mwao walijeruhiwa.
Ripoti nyingine zinasema kuwa askari usalama wamekuwa wakishambulia maeneo ya makazi katika pembe tofauti za nchi hiyo na kuwatia nguvuni watu wanaoshukiwa kushiriki kwenye maandamano ili kwa njia hiyo kujaribu kuzima maandamano dhidi ya utawala wa Aali Khalifa. Lakini wananchi wa nchi hiyo ambao wamekuwa wakiendesha kwa amani maandamano hayo yaliyoanza tarehe 14 Februari 2011, wameazimia kuyaendeleza hadi watakapouangusha utawala huo. Wabahraini pia jana Ijumaa walifanya maandamano katika miji mbalimbali dhidi ya utawala huo.
Akizungumza hivi karibuni na televisheni ya al- Alam kuhusiana na hali ya Bahrain, Hadi al-Musawi, mkuu wa idara ya uhuru na haki za binadamu ya chama cha al-Wifaq amesema hali ya kisiasa ya nchi hiyo inazidi kuharibika kutokana na kiburi na upuuzaji wa utawala wa nchi hiyo kuhusu matakwa halali ya wananchi.
Wapinzani wa Bahrain wanasema kuwa Marekani na utawala wa Saudi Arabia ndio wanaohusika na jinai zinazotekelezwa na utawala wa Bahrain dhidi ya wananchi wa nchi hiyo.
Ni zaidi ya mwaka mmoja sasa ambapo matakwa halali ya wananchi wa Bahrain yamekuwa yakikabiliwa na jinai zinazotekelezwa kwa ushirikiano wa utawala wa Aali Kalifa, Aali Saud na Marekani. Licha ya hayo wananchi wa Bahrain wameapa kuendelea na maandamano yao ya amani dhidi ya utawala huo hadi watakapotekelezewa matakwa yao yote.


994601
captcha