IQNA

Kumjua Bibi Fatma katika Uislamu; sharti muhimu la kuifahamu vyema dini

17:50 - April 29, 2012
Habari ID: 2314500
Muhammad Ridha Qezelsufla, mwambata wa utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Sierra Leone amesema kwamba kwa kuzingatia hadithi ya Mtume Muhammad (saw) inayosema kwamba 'Fatima ni sehemu ya mwili wangu,' tunaelewa kwamba ufahamu na utekelezaji wa mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu na pia umaanawi wake huwa na upungufu, ikiwa hatutafahamu na kutambua vyema nafasi ya Bibi Fatuma (as) binti ya Mtume Mtukufu (saw) katika Uislamu.
Bwana Qezelsufla aliyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza katika kikao cha 'Bibi Fatma (as) na Mwamko' kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kitengo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko mjini Free Town, kwa ushirikiano wa taasisi kadhaa za Kiislamu na kuhudhuriwa na idadi kubwa ya wanawake wasomi wa Kiislamu. Amesema kutumika kwa wingi jina na lakabu za Bibi Fatma miongoni mwa mabinti na wanawake wa Kiislamu wa Sierra Leone ni ishara ya wazi kwamba wanawake hao wanawapenda Watu wa Nyumba ya Mtume (saw).
Ameelezea matumaini yake kwamba wanawake wa Sierra Leone watatekeleza vyema mafundisho ya bibi huyo mtukufu wa Kiislamu katika maisha yao ya kila siku ili kuwa mfano bora kwa Waislamu na wasio Waislamu na vilevile kupata saada ya humu duniani na huko Akhera. Makumbusho hayo yaliendelea kwa kusomwa makala na hutuba mbalimbali za kusifu na kubainisha maisha ya Bibi Fatma, zilizotolewa na wanawake tofauti wa Kiislamu wanaojishughulisha na masuala ya kiutamaduni katika vituo vya kielimu vya Sierra Leone. 995592
captcha