IQNA

Kasisi mwovu wa Marekani achoma tena Qur'ani Tukufu

16:58 - April 30, 2012
Habari ID: 2315389
Kwa mara nyingine tena Kasisi Terry Jones wa Kanisa la Dove World Outreach Center katika mji wa Gainsville jimboni Florida Marekani, amechoma moto Qur'ani Tukufu.
Hii ni mara ya pili kwa kasisi huyo mwovu kuchukua hatua kama hiyo ya kuvunjia heshima kitabu kitakatifu cha Waislamu. Kabla ya kuchoma moto kitabu hicho pamoja na picha ya mtu aliyetajwa kuwa ni ya Mtume Muhammad (saw), Kasisi Jones alisoma taarifa akitoa sababu za kuchukua hatua hiyo ya kipumbavu dhidi ya matukufu ya kidini. Hata hivyo, kitendo chake hicho mara hii hakikuakisiwa sana na vyombo vya habari vya Marekani kama ilivyokuwa katika kitendo cha kwanza.
Mwaka uliopita Terry Jones alitishia kuchoma moto Qur'ani Tukufu katika makumbusho ya matukio ya kigaidi ya Septemba 11 nchini Marekani lakini alilazimika kutotekeleza tishio hilo kutokana na mashinikizo ya kimataifa.
Hata hivyo, kitendo chake cha kuchoma moto Qur'ani Tukufu mwezi Machi uliopita kiliamsha hasira ya Waislamu duniani na hasa nchini Afghanistan ambako Waislamu wa nchi hiyo walifanya maandamano makubwa ya kulalamikia kitendo hicho. Hii ni katika hali ambayo Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon, kidhahiri ilikuwa umemwomba kasisi huyo asichome moto Qur'ani kwa kuhofia matokeo yake mabaya katika ulimwengu wa Kiislamu na hasa nchini Afghanistan ambako nchi hiyo ina askari jeshi wengi. Ukweli ni kwamba watawala wa Marekani kabla ya kuwa walipinga kitendo cha kuchomwa Qur'ani kutokana na ukiukaji wake wa thamani za kidini, walikipinga kutokana na kuhofia athari zake mbaya kwa askari jeshi wao wanaohudumu katika nchi za Kiislamu. Licha ya kuwa Rais Barrack Obama wa Marekani aliahidi katika siku za mwanzo za kuingia madarakani kwamba angetekeleza sera zinazoheshimu thamani na haki za Waislamu, lakini hatua zake za hivi karibuni dhidi ya Waislamu zinathibitisha wazi kwamba amekiuka ahadi hizo. Kwa kisingizio cha eti kulinda uhuru wa mtu binafsi na hasa wa kujieleza, watawala wa ngazi za juu wa Marekani hawajachukua hatua yoyote ya kuzuia vitendo vya aibu na dharau vinavyotekelezwa na kasisi huyo wa Marekani dhidi ya Uislamu na Waislamu. Hii ni katika hali ambayo iwapo jambo kama vile holocaust litatiliwa shaka ndogo tu nchini humo au nchi nyingine za Magharibi, viongozi wa nchi hizo huchukua hatua kali za kupambana na hata kuwafunga jela watu wanaotilia shaka suala hilo.
Ni wazi kuwa propaganda na ukandamizaji wote ambao umekuwa ukitekelezwa na nchi hizo dhidi ya Uislamu kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi sasa umechukua mkondo mpya. Vyombo vya usalama vya nchi za Magharibi vimekuwa vikifanya ujasusi na kukiuka wazi uhuru wa Waislamu kwa kusikiliza kwa siri mazungumzo yao ya faragha, na wala serikali za nchi hizo zinazodai kutetea uhuru wa mtu binafsi na wa umma, huwa hazichukui hatua zozote za kukabiliana na jambo hilo. Licha ya hayo, vyombo vya habari vya Magharibi na hasa ya Marekani, vimekuwa vikiendesha propaganda za kiuadui na kuzusha hofu dhidi ya Waislamu wanaoishi katika nchi hizo na hivyo kuwafanya waishi daima katika hali ngumu na ya woga.
Kwa ufupi ni kuwa vitendo vya kuzusha hofu dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini Marekani, vimepelekea maadui wa Uislamu nchini humo kukanyaga wazi matukufu ya Kiislamu na kuwabagua Waislamu kwa kila njia. Hatua ya hivi karibuni ya Terry Jones, kasisi mwenye misimamo mikali ya ubaguzi wa kidini, ya kuchoma moto Qur'ani Tukufu ni dalili inayothibitisha wazi siasa za uadui wa serikali ya Marekani dhidi ya Uislamu na uungaji mkono wake usio wa moja kwa moja kwa vitendo vya kasisi huyo. Na hasa tukitilia maanani kwamba hakuna kiongozi yoyoye wa Marekani aliyeonya wala kukemea kitendo cha hivi karibuni cha kasisi huyo mwovu. 996467
captcha