Hatua ya Riyadh ya kufunga ubalozi wake mjini Cairo na balozi zake ndogo katika miji ya Alexandria na Suez imekuja baada ya maelfu ya wananchi wenye hasira wa Misri kufanya maandamano hivi karibuni mbele ya ubalozi na balozi ndogo za Saudi Arabia ili kuonyesha hasira zao dhidi ya siasa za Riyadh za kuingilia masuala ya ndani ya nchi yao.
Kwa muda sasa wananchi wa Misri wamekuwa wakilalamikia siasa za Riyadh za kuingilia masuala ya ndani ya nchi yao na hata wamewahi kusikika wakisema kuwa wanataka balozi wa Saudia afukuzwe nchini mwao.
Wananchi wa Misri ambao wana hisia kali sana mbele ya hatua yoyote ile inayohatarisha kufikiwa malengo ya mapinduzi yao, wanaziona siasa za Riyadh kuwa ni hatari sana kwa mapinduzi yao yaliyomg'oa madarakani dikteta Hosni Mubarak. Wananchi wa Misri wanalalamika kuwa, kama ambavyo viongozi wa Saudi Arabia wamekuwa wakiwahifadhi na kuwakingia kifua watawala madikteta wa nchi nyinginezo, wanawaunga mkono pia watu wanaopinga mapinduzi ya wananchi wa Misri. Vile vile wanasema, viongozi wa Riyadh wanaunga mkono mirengo ya watu wenye mielekeo ya Magharibi wanaopinga Uislamu nchini Misri.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, viongozi wa Saudi Arabia wana wasiwasi mkubwa wa kuingia madarakani viongozi wenye mielekeo ya Kiislamu nchini Misri hasa Ikhwanul Muslimin kwani viongozi hao hawatakubali kuburuzwa kwenye mazungumzo yasiyo na tija na utawala wa Kizayuni na jambo hilo linakinzana na siasa za Saudia za kufanya mazungumzo na Wazayuni. Jambo jengine linaloonekana kuwakasirisha wananchi wa Misri ni jinsi viongozi wa Saudia hasa watu wa ukoo wa kifalme wanavyowanyanyasa wananchi wa Misri. Inadaiwa kuwa mashirika ya Saudia yanayomilikiwa na ukoo wa kifalme wa Aal Saud kwa muda mrefu yamejipenyeza katika sekta tofauti za kiuchumi za Misri yakiendelea kupora utajiri wa nchi hiyo. Wananchi hao wa Misri wanasema kuwa, mashirika hayo yanazidisha migogoro ya kiuchumi na umaskani nchini Misri kutokana na kutoa mishahara isiyokidhi haja na kutofikiria kabisa kuwanyanyua kiuchumi wananchi wa nchi hiyo.
Malalamiko ya wananchi wa Misri yalishadidi baada ya viongozi wa Saudia kumtia mbaroni hivi karibuni mwanasheria mmoja wa Misri na mkewe, jambo ambalo limetumiwa na wananchi wa Misri kama fursa ya kuzidi kuonesha malalamiko yao dhidi ya siasa za Riyadh za kungilia masuala ya ndani ya nchi yao.
Kiujumla ni kuwa siasa za Saudi Arabia haziwafurahishi wananchi wa nchi nyingi za Kiarabu zinazoshuhudia harakati za kimapinduzi dhidi ya tawala vibaraka na iwapo viongozi wa Saudia wataendelea na siasa hizo, basi ni wazi kuwa watazidi kuipotezea itibari nchi hiyo mbele ya fikra za walio wengi katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu.
996394