Allamah Sayyid Hassan Annamr amelaani vikali hatua ya Kasisi Terry Jones wa Marekani ya kukariri kitendo cha kuchoma moto nakala za Qur'ani na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni mwenendo muovu unaolenga umma wa Kiislamu.
Amemtaja Kasisi Terry Jones kuwa ni mtu mwenye chuki na uhasama dhidi ya Uislamu na kusema kuwa viongozi wa serikali ya Marekani pia wamechangia katika makosa hayo ya kuchomwa moto nakala za Qur'ani Tukufu kwa sababu ya kukataa kuzuia uhalifu huo.
Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kishia wa Saudia amesema kuwa iwapo taasisi husika zingemchukulia hatua kasisi huyo kwa mujibu wa sheria za kimataifa zinazokataza kuvunjia heshima matukufu ya kidini, hapana shaka kwamba asingekariri kitendo hicho kiovu.
Sayyid Hassan Annamr amewataka viongozi wa Marekani wasitosheke na kulaani kwa maneno matupu kitendo cha kuchomwa moto nakala za Qur'ani na wachukua hatua za kivitendo dhidi ya jinai hiyo ambayo imejeruhi hisia za Waislamu zaidi ya bilioni moja na nusu kote duniani.
Vilevile amezitaka nchi za Kiislamu kuchukua hatua na kulaani vikali kitendo hicho kiovu. Amesisitiza kwamba ili kuonyesha upinzani wao dhidi ya uhalifu huo, nchi za Kiislamu zinapaswa kuwarejesha nyumbani angalau kwa muda mabalozi wao walioko nchini Marekani. 998748