IQNA

Mtafiti wa masuala ya Qur'ani wa Iraq:

Wasiwasi wa kuenea kwa kasi dini ya Kiislamu ndio sababu ya kuchomwa moto Qur'ani

18:50 - May 02, 2012
Habari ID: 2317213
Maudhui ya kuvunjiwa heshima kitabu kitakatifu cha Mwenyezi Mungu, Qur'ani na kukaririwa vitendo hivyo viovu dhidi ya kitabu kitakatifu zaidi cha Waislamu na itikadi zao, vinatokana na woga wa Wamagharibi kuhusu maendeleo ya pande zote ya Waislamu na hofu yao kuhusu wimbi la wasio Waislamu kuingia katika dini hiyo.
Hayo yamesemwa na Ali Ramadhan al Ausi, mtafiti wa masuala ya Qur'ani wa Iraq na Mkurugenzi wa Kitengo cha Lugha ya Kiarabu cha Kituo cha Kiislamu cha Uingereza. Al Ausi ameiambia IQNA kwamba maadui na jamii za Magharibi walioona maendeleo ya Uislamu na uwezo wa Waislamu wa kutatua matatizo ya zama hizi, wameamua kufanya njama za kuchafua sura na jina la dini hiyo na inasikitisha kwamba wamelenga thamani za Kiislamu na matukufu yake kama Qur'ani Tukufu, misikiti, vazi la hijabu na matukufu mengine.
Amesema taathira kubwa ya Qur'ani kwa wasio Waislamu, uwezo wake wa kuwavutia katika dini ya Kiislamu na woga kwamba mustakbali utakuwa wa Uislamu na Waislamu ni miongoni mwa sababu za vitendo viovu vya kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu na thamani za Kiislamu na kukaririwa vitendo hivyo viovu katika jamii za nchi za Magharibi.
Amesema kuwa inasikitisha kwamba vitendo hivyo vimekuwa vikikaririwa na baadhi ya watu na makundi yenye misimamo mikali lakini hakuchukuliwi hatua yoyote ya maana ya kukabiliana nao isipokuwa kutoka Iran na Afghanistan. Amesisitiza kuwa pale nchi nyingine zinapolalamikia uhalifu huo basi hatua hizo huwa dhaifu.
Mwandishi huyo amesema Marekani imekuwa na msimamo wa kindumakuwili kuhusu uhalifu huo wa kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu ambao umewakasirisha mno Waislamu kote duniani na kuzusha uhasama kati ya wafuasi wa dini mbalimbali. Amesema katika upande mmoja Washington inadai kuwa inapinga vitendo hivyo na wakati huo huo inavihalalisha kwa kisingizio cha kutetea uhusu wa kujieleza. Ali Ramadhan al Ausi amesisitiza kuwa hapana shaka kwamba kama Muislamu angefanya kitendo kama hicho basi msimamo wa viongozi wa nchi za Magharibi utakuwa tofauti kabisa. 997975


captcha