IQNA

Umoja wa Mataifa kuchunguza ukiukwaji wa haki za binaadamu Bahrain

16:33 - May 17, 2012
Habari ID: 2328013
Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kujadili kadhia ya haki za binaadamu nchini Bahrain katika kikao chake kijacho mjini Geneva Uswisi.
Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, kikao hicho kitaanza Mei 21 hadi Juni ambapo suala la ukiukwaji haki za binaadamu Bahrain litajadiliwa siku ya kwanza.
Hivi karibuni katibu Mkuu wa Mrengo wa Kiislamu wa al Wifaq nchini Bahrain amesema kuwa, kuwepo muungano kati ya Saudi Arabia na Bahrain hakuwezi kusimamisha mapinduzi ya wananchi wa Bahrain.
Jameel Kadhim Katibu Mkuu wa Mrengo wa Kiislamu wa al Wifaq aliyasema hayo hapo jana katika mahojiano na televisheni ya Al Alam na kuongeza kuwa, dalili zinaonyesha kuwa nchi mbili yaani Saudi Arabia na Bahrain zinakusudia kuanzisha muungano na kwamba hatua hiyo katu haitaweza kusimamisha harakati za mapinduzi za wananchi wa Bahrain. Ameongeza kuwa, malengo ya utawala wa Aal Khalifa katika kuanzisha muungano huo ni kupata fursa ya misaada kutoka kwa nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi kwa ajili ya kufuta mapinduzi ya wananchi wa nchi hiyo.
Kwa upande wake Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limekosoa ukandamizaji unaoendelea kufanywa na serikali ya Bahrain kwa uungaji mkono wa Marekani dhidi ya wapinzani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Amnesty International nchini Marekani Suzanne Nossel amekosoa vikali ukandamizaji unaofanywa na serikali ya kifalme ya Bahrain dhidi ya wapinzani na wananchi wanaopinga utawala wa Aal Khalifa. Amesema kuwa vitendo vya kuendelea kuwatia nguvuni wapinzani na wananchi wanaoandamana dhidi ya serikali, kutoa hukumu kali dhidi ya wapinzani na kuhukumiwa kwao katika mahakama zisizokuwa za kiadilifu haviwezi kukubalika. Suzanne Nossel ameongeza kuwa serikali ya Bahran inaficha mambo mengi yanayohusiana na machafuko yanayoendelea nchini humo.
1009832
captcha