Kanali ya Press TV imedokeza kuwa baada ya kushindwa kuiangusha serikali halali ya Rais Bashar al Assad, wakuu wa Washington na Riyadh sasa wako katika mbio za kutekeleza njama mpya. Awali kabisa wanataka kuonyesha kuwa hakuna amani itakayopatikana Syria pasina idhini ya Marekani na pili ni kuwachosha wafuasi wa rais Assad ili waache kumuunga mkono.
Wakati huo huo Katika hatua ya kuendeleza mpango wa marekebisho ya kisiasa alioutangaza Rais wa Syria Bashar al Asad, kwa mara nyingine hivi karibuni rais huyo ametoa amri ya kuundwa chombo cha mahakama ya katiba ya nchi hiyo.
Rais Bashar al Asad alitoa amri ya kuundwa chombo cha mahakama kuu ya katiba siku ya Jumapili ya tarehe 13 Mei mwaka huu. Mahakama hiyo inatarajiwa kuundwa na mihimili saba mikuu na itafanya kazi kwa muda wa miaka minne. Hii ni katika hali ya kwamba katika kipindi cha miaka hiyo minne katiba itakuwa na uwezekano wa kufanyiwa marekebisho. Kwa msingi huo mkuu wa mahakama kuu ya katiba atachaguliwa na rais na atafanya kazi kwa uhuru. Aidha kwa mujibu wa sheria ni kwamba, watumishi wa mahakama hiyo ni lazima kwa uchache wawe na miaka 15 katika shughuli za ukadhi, au katika kufundisha sheria na kwamba rais pia anayo mamlaka ya kuongeza idadi ya watumishi katika chombo hicho. Kazi muhimu ya chombo hicho ni kufungua mlango kwa matakwa ya wagombea urais nchini humo sambamba na kuwa na uwezo wagombea hao kutoa dukuduku zao katika masuala yanayohusiana na usalama wa uchaguzi wa urais na kadhalika. Ni wazi kwamba, kuundwa chombo hicho chenye lengo la kufuatilia uchaguzi wa urais nchini Syria kunaleta bishara njema kwa raia wote wa Syria hasa kwa kuzingatia kuwa, mpango wa kuanzishwa chombo kama hicho chenye lengo la kusimamia uchaguzi wa rais ndio mara ya kwanza kuwepo tangu nchi hiyo ilipojipatia uhuru wake. Kabla ya kutangazwa tume hiyo ya kisheria (yaani mahakama kuu ya kikatiba nchini Syria), tayari rasimu ya katiba hiyo ilikuwa imeandaliwa. Rasimu hiyo iliandikwa kwa mujibu wa katiba mpya ya sasa ya nchi hiyo ambayo ilipigiwa kura na wananchi wa Syria tarehe 26 Februari mwaka huu.
Wakati huo huo matokeo ya uchaguzi wa bunge la nchi hiyo ambao nao ni natija ya katiba mpya ya sasa ya nchi hiyo yanatazamiwa kutangazwa hii leo. Kwa amri ya Rais Bashar al Asad wa Syria hadi sasa sheria za vyama, vyombo vya habari, magazeti, chaguzi za idara, chaguzi za nchi na katiba ya nchi hiyo tayari zimefanyiwa marekebisho. Pamoja na mafanikio hayo makubwa ya marekebisho yaliyofanywa na rais wa nchi hiyo, bado Wamagharibi wakiongozwa na Marekani wanaendeleza harakati za machafuko zaidi nchini Syria. Hadi sasa Marekani imetangaza wazi kuhusika na uvunjifu wa amani nchini humo kwa kuyafadhili kwa hali na mali makundi ya kigaidi ili kwa njia hiyo waweze kumuweka Bashar al Asad rais wa nchi hiyo katika mashinikizo magumu ya kisiasa.
Katika fremu hiyo hivi karibuni Syria ilishuhudia mashambulizi ya milipuko mikubwa ambayo ilipelekea kuuawa idadi ya watu wengi na wengine kujeruhiwa. Milipuko hiyo inafanyika huku pande mbili hasimu zikiwa zilikwishatia saini mpango wa amani wa kipengele nambari 6 wa Kofi Annan, mjumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu katika kadhia ya Syria. Hatahivyo pamoja na kutiwa saini mpango huo bado amani haijarejea nchini humo.
1009455