IQNA

Fifa yakaribisha mavazi mapya ya wanamichezo wa kike wa Kiislamu

17:59 - May 21, 2012
Habari ID: 2330993
Aina mpya ya nguo zinazopaswa kuvaliwa na wanamichezo wa kike wa Kiislamu wanaotaka kushindana mashindano ya kimataifa imevutia na kuwaridhisha maafisa wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu, Fifa.
Kwa mujibu wa Globe and Mail, mtindo huo wa nguo umebuniwa na msanii mmoja wa Canada anayejulikana kwa jina la Sayyida Jawad. Kwa mujibu wa ripoti hiyo bibi huyo wa Kiislamu aliwasilisha nguo hizo kwa Ali al-Hussein bin Ali, naibu mkuu mpya wa Fifa anayeshughulikai masuala ya tiba na mavazi. Wataalamu wa mambo wanasema kuwa vazi hilo la kuvutia linawawezesha wanawake wa Kiislamu kushiriki kwenye michezo mbalimbali wanayopenda bila kuvunja sheria zao za kidini kuhusiana na umuhimu wa kusitiri sehemu zao za mwili zisizopasa kuonekana hadharani. Msanii huyo wa Kiislamu aliye na umri wa miaka 28 amesema amechukua uamuzi wa kufuma vazi hilo baada ya kusikia habari ya kuhuzunisha kwamba wanawake watano wa Kiislamu waliokuwa wamevalia hijabu walizuiwa kushiriki kwenye michezo ya kuwania ubingwa wa mchezo wa taekwondo au binti mwingine Kiislamu wa umri wa miaka 11 kutoka Ottawa Canada kutokana na sababu hiyohiyo. Amesema wanawake wote wawe ni wa Kiislamu au wasio Waislamu wanapasa kupewa fursa sawa za kushiriki katika michezo inayowavutia. Hata hivyo msemaji wa Fifa amesema kwamba hijabu itaruhusiwa tu kutumika katika viwanja vya mpira wa miguu pale itakapoidhinishwa rasmi na wakuu wa shirikisho hilo. 1012507
captcha