Kwa mujibu wa tovuti ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu, Jumatano ya leo ya Mwezi Mosi Rajab imesadifiana na kumbukumbu za Siku ya Kuzaliwa Imam Muhammad Baqir AS mmoja wa wajukuu watukufu wa Mtume Muhammad SAW.
Siku hii pia imesadifiana na tarehe 3 Khordad, (mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia), siku ya kukumbuka wanamapambano wa Iran walipoukomboa mji wa Khoramshahr uliokuwa umetekwa na kukaliwa kwa mabavu na vikosi vya utawala wa wakati huo vya Iraq.
Kwa mnasaba wa tukio hilo, wanachuo wa Chuo Kikuu cha maafisa wa kijeshi cha Imam Husain AS wamefanya sherehe maalumu za kumaliza masomo zilizohudhuriwa na Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei.
Mwanzoni mwa kuingia kwake kwenye Chuo Kikuu hicho, Amirijeshi Mkuu wa majeshi yote ya Iran amekwenda kwenye maziara ya mashahidi na kuwasomea Faatiha na dua za kheri mashahidi hao wa kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu.
Baada ya hapo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekagua vikosi mbali mbali vilivyokuwa vimepanga paredi kwenye uwanja wa Chuo Kikuu hicho.
Katika hotuba yake mbele ya washiriki wa sherehe hizo, Ayatullah Udhma Khamenei ameitaja heshima, uwezo na nguvu zinazoongezeka kila leo za taifa la Iran kuwa zinatokana na kusimama kwake kidete na imara taifa hili katika njia ya bay'a na kujisalimisha kikamilifu kwa Mwenyezi Mungu.
Aidha amesema, taifa lililoko mstari wa mbele la Iran, litaongeza kasi yake ya kujiletea maendeleo makubwa zaidi na kusimamisha uadilifu sambamba na kupambana vilivyo na kambi ya dhulma, mabeberu na waistikbari katika muongo huu wa maendeleo na uadilifu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Amesema, licha ya kwamba madola ya kibeberu yanajionesha kwa walimwengu kuwa yana nguvu, lakini ukweli ni kwamba madola hayo yanazidi kudhoofika na nguvu zao zinazidi kudidimia kadiri siku zinavyosonga mbele.
Aidha amesisitiza kwamba, taifa la Iran lina matumaini mazuri kuhusu mustakbali wake na kuongeza kuwa, vijana wa Kiirani wenye kuliletea fakhari taifa lao na ambapo nchi hiyo nayo ni mali yao wenyewe, wana jukumu la kuwa mstari wa mbele kwa ajili ya kuliletea maendeleo taifa hili na hatimaye kuweza kuuletea fakhari na mafanikio makubwa umma wote wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, njia ya kuelekea kwenye vilele vya juu kabisa vya saada na ufanisi imekuwa wazi hivi sasa kutokana na jitihada kubwa ya vizazi vilivyopita vya Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kwa kusema: Tab'an kuweko wazi njia hiyo hakuna maana kwamba tabu, mashaka na uzito wote umeondoka, bali inabidi njia hiyo iendelezwe kwa kudumisha istikamana na kusimama kidete.
Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amevisifu vikosi vya ulinzi vya Iran iwe ni Jeshi au Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH au jeshi la Basiji kutokana na kuwa kwao imara katika bay'a na kujisalimisha kwao vilivyo kwa Mwenyezi Mungu na kuongeza kuwa: Wakati wa vita vya kujihami kutakatifu, vikosi vya vya ulinzi vya Iran vilipata uzoefu mkubwa na tajiriba muhimu mno na ya kubakia milele na inabidi uzoefu na tajiriba hiyo itumike wakati wote kwa ajili ya kuangaza njia ya mustakbali bora wa taifa.
Katika sherehe hizo, Meja Jenerali Muhammad Ali Jafari, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH ametoa ripoti kuhusu jinsi vinavyofanya kazi vikosi aina nne vya SEPAH na taasisi ya Basiji, na jinsi unavyotiwa nguvu uwezo wao chini ya mwavuli wa mipango ya kiulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Meja Jenerali Jafari amezungumzia pia ratiba za mafunzo ya jeshi la SEPAH chini ya kivuli cha mfumo mzima wa malezi na mafunzo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Naye Bw. Morteza Safari, Kamanda wa Chuo Kikuu cha Maafisa wa Kijeshi cha Imam Husain AS ametoa ripoti kuhusu ratiba za kielimu, kimafunzo na kijeshi za chuo hicho mbele ya Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Vile vile makamanda kadhaa, wahadhiri, wanachuo, watu wanaojitolea kwenye njia ya haki na familia za mashahidi wa jeshi la SEPAH wamepewa zawadi kwenye sherehe hizo na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Aidha wawakilishi wa wanachuo na wanafunzi wengine wa chuo hicho wamepata fakhari ya kupandishwa vyeo. Mwishoni mwa sherehe hizo, vikosi mbalimbali vimepita kwa gwaride mbele ya Amirijeshi Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei.
1015144