IQNA

Uchaguzi wa Rais nchini Misri na Mustakabali wa Harakati ya Kiislamu

11:43 - May 24, 2012
Habari ID: 2332997
Kwa mara nyengine Misri inaingia kwenye mtihani nyeti unaogusa hatima na mustakabali wa nchi hiyo. Hakuna shaka yoyote kuwa kufanyika uchaguzi wa rais wa Misri ulioanza jana leo kunaweza kuhesabiwa kuwa nukta ya kilele cha mageuzi katika historia ya mwamko wa Kiislamu ulioanza nchini humo mwaka uliopita.
Jana na leo wananchi wa Misri wanaelekea vituo vya kupigia kura kumchagua rais wao mpya ambapo kwa mujibu wa tume ya uchaguzi ya nchi hiyo zaidi ya watu milioni 50 kati ya wananchi wote milioni 80 wametimiza masharti ya kupiga kura.
Miongoni mwa mambo yanayoshuhudiwa kwa uwazi zaidi katika uchaguzi huo wa kwanza huru wa rais tangu ulipoangushwa utawala wa kidikteta wa Hosni Mubarak ni kushiriki karibu mirengo yote yenye mielekeo tofauti ya kisiasa nchini humo. Wagombea 13 ambao majina yao yamepitishwa na tume ya uchaguzi wanatoka kwenye mirengo yenye mitazamo na mielekeo inayotafautiana. Wagombea wanne wana mielekeo ya Kiislamu, watatu wana sera za utaifa, wanne ni wawakilishi wa mitazamo ya kimagharibi na wagombea wawili wana mielekeo ya mrengo wa kushoto. Muhammad Mursi na Abdul Mun'im Abul Futuh ni wagombea wenye mielekeo ya Kiislamu, wakati Amr Mousa anahesabiwa kuwa mtu mwenye misimamo ya kiliberali.
Hakuna shaka kuwa mchuano mkali utakuwa baina ya kambi hizo mbili zenye mitazamo hiyo ya kifikra na kisiasa. Wamisri wa matabaka ya chini na ya kati wanavutiwa zaidi na wagombea wenye mielekeo ya Kiislamu wakati wasomi na majenerali wa kijeshi wanamuunga mkono Amr Mousa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Unyeti na umuhimu wa uchaguzi wa rais wa Misri umeongezeka maradufu hasa kutokana na kuwepo hofu na wasiwasi wa muda mrefu katika duru za kisiasa za nchi hiyo wa kufanyika uchakachuaji na udanganyifu kwa maslahi ya mgombea fulani.

Kwa wananchi wa Misri ambao wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu kuundwa serikali waliyoichagua kwa ridhaa yao, kung'atuka majenerali wa jeshi katika hatamu za uongozi wa kisiasa na za utendaji ni jambo muhimu sana kwa wananchi hao, lakini kwa upande wa wanajeshi ambao kwa miaka na miaka wamekuwa wakichukuliwa kuwa moja ya nguzo na mihimili muhimu ya madaraka katika mfumo wa kisiasa wa Misri, tukio hilo litakuwa kumbukumbu chungu mno kwao.

Baraza Kuu la Kijeshi ambalo ndio chombbo kikuu cha utawala, hivi sasa lina wasiwasi wa wanajeshi kuwekwa kando ya ulingo wa siasa na hatamu za madaraka endapo Wamisri wataamua kumchagua mgombea mwenye misimamo huru na mielekeo ya Kiislamu.

Hivi sasa mrengo wenye mielekeo ya Kiislamu ndio wenye viti vingi bungeni. Na hali ni hiyo hiyo pia katika baraza la kutunga Katiba. Baraza Kuu la vikosi vya ulinzi halipendi kuona yale yaliyotokea kwenye chaguzi za Bunge na baraza la kutunga Katiba yanajirudia katika uchaguzi wa rais. Kwa sababu hiyo kama zilivyo nchi za Magharibi, Marekani na baadhi ya nchi za Kiarabu katika eneo linatamani kuona rais mpya wa Misri anakuwa mtu mwenye mielekeo ya utaifa na ya kiliberali. Hamu na utashi huo unazidisha shaka na wasiwasi juu ya namna zoezi la uchaguzi wa leo litakavyoendeshwa na matokeo yake yatakavyotangazwa. Kutokana na kuchelea hatua hatari zinazoweza kuchukuliwa na Baraza Kuu la vikosi vya ulinzi na pia maafisa wa serikali, makundi ya kisiasa nchini Misri yameamua kuunda tume za usimamizi ili kuweza kufuatilia kwa karibu zaidi yale yatakayokuwa yakijri katika vituo vya kupigia kura. Hakuna shaka kuwa matokeo ya uchaguzi wa rais Misri utakuwa na nafasi muhimu katika kuainisha muelekeo wa harakati ya mwamko wa Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika.
1014865
captcha