IQNA

Mamilioni ya Wamisri wapiga kura katika uchaguzi wa Rais

11:50 - May 24, 2012
Habari ID: 2333011
Mamilioni ya wananchi wa Misri jana na leo wameshiriki katika zoezi la kwanza la uchaguzi wa kidemokrasia wa Rais.
Jana ilikuwa siku ya kwanza ya uchaguzi huo wa siku mbili na taarifa zinasema kuwa, mamilioni ya wapiga kura walimiminika kwenye vituo vya kupigia kura kwa ajili ya kumchagua rais wa baadaye wa nchi hiyo.
Watu milioni 50 wametimiza masharti ya kupiga kura kote nchini Misri. Vituo 13,000 vya kupigia kura vimewekwa katika kona mbalimbali za mikoa 27 ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa mbili asubuhi na kufungwa saa tatu usiku kwa saa za nchi hiyo baada ya kuongezwa saa moja. Uchaguzi huo unaendelea leo na kazi ya kuhesabu kura itaanza mara baada ya kumalizika zoezi la upigaji kura.
Wagombea 13 wanashiriki kwenye kinyang'anyiro hicho huku wagombea watatu wakipewa nafasi kubwa ya kushinda, yaani mgombea wa kundi la Ikhwanul Muslimin, Muhammed Mursi, mgombea wa kujitegemea Abdul Mun'im Abul Futuh na Katibu Mkuu wa zamani wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Amr Moussa.
Mursi aliongoza katika kura zilizopigwa na Wamisri walioko nje ya nchi, kwa kupata asilimia 40 ya kura za uchaguzi huo uliofanyika siku ya Ijumaa ya tarehe 11 mwezi huu wa Mei katika balozi za Misri kwenye nchi mbalimbali duniani.
Endapo hakutokuwa na mgombea atakayepata kura za kumwezesha kutangazwa mshindi, duru ya pili ya uchaguzi huo itafanyika tarehe 16 na 17 za mwezi ujao wa Juni.
1014939
captcha