IQNA

Imam Khamenei: Wabunge wafikirie tu majukumu yao mbele ya Mwenyezi Mungu

12:00 - May 28, 2012
Habari ID: 2335923
Bunge la Tisa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran linalojulikana kwa jina la Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, limefunguliwa rasmi Jumapili hii mjini Tehran kwa ujumbe wa Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Bunge la Tisa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran linalojulikana kwa jina la Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumapili) limefunguliwa rasmi kwa ujumbe wa Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Matini kamili ya ujumbe huo ambao umesomwa na Hujjatul Islam Walmuslimin Muhammadi Golpeygani, Mkuu wa Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika sherehe za ufunguzi wa bunge hilo ni kama ifuatavyo:

Bismillahir Rahmanir Rahim

Kuanza kufanya kazi duru ya nne ya chombo cha kutunga sheria cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran - kwa uwezo na mapenzi ya Mwenyezi Mungu, Mwingi wa hekima na Mwenye nguvu - ni ujumbe muhimu na mzito unaotolewa na taifa la Iran kwa dunia ya leo na ni uhakika wenye kubakia milele katika fikra za walio wengi za mataifa ya dunia. Ushindi wa irada ya taifa mbele ya wimbi kubwa la uadui wa maadui, jengo madhubuti na imara la mfumo uliotokana na Mapinduzi ya Kiislamu, nafasi ya kipekee na isiyo na mithili ya imani, tabasuri na muono wa mbali katika kutoa muelekea kwa mfumo wa maisha ya mwanadamu na mustakbali wa taifa, na hatimaye, kutoa taswira sahihi ya taifa ambalo limeonesha kwa mara ya kwanza mfumo mpya wa demokrasia ya kidini, si kwa maneno bali kwa jihadi na jitihada kubwa na hivyo kuweza kubatilisha madai ya kutengwa dini katika maisha ya watu ndani ya jamii, ni miongoni mwa uhakika huo wenye taathira za kudumu.
Kufanikiwa taifa la Iran kufikisha ujumbe huo muhimu, mzito na wenye kuleta mwamko kwa fikra za walio wengi duniani, ni baraka na neema nyingine za Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu na Mwenye huruma, Ambaye katika kipindi chote hiki kilichojaa mashaka na changamoto, kamwe hakuliacha mkono bali wakati wote amekuwa akilisaidia na kuliongoza kwenye njia sahihi taifa la waumini na wanajihadi la Iran. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa dhati ya nyoyo zetu na tunamsujudia Yeye katika sijda ya shukru, kuonyesha shukrani zetu kubwa Kwake.
Vile vile ni wajibu wangu kulishukuru na kulipongeza taifa kubwa na linalojenga historia la Iran kwa udhati wa moyo wangu na ninawashukuru pia wananchi wote wa Iran kwa kujitokeza kwao katika wakati mwafaka kwenye somo hili lenye kubakia milele na kuweza - kama ilivyo kawaida yao - kuonesha muono wao wa mbali na welewa wao sahihi kuhusu zama wanazoishi.
Vile vile ni wajibu wangu kuwashukuru viongozi na maafisa wote wa Wizara ya Mambo ya Ndani na Baraza la Kulinda Katiba na taasisi na vyombo vyote vilivyofanikisha kufanyika uchaguzi wa Bunge hasa vyombo vya habari vya taifa na maafisa wa kusimamia usalama na amani, pamoja na shakhsia wote wa kidini na kisiasa ambao kila mmoja amesaidia kwa namna moja au nyingine kufanikisha hamasa hiyo ya watu wote (yaani uchaguzi wa Bunge). Vile vile ni wajibu kwangu kuwashukuru kwa udhati wa moyo wangu, Wabunge wote wa Bunge la Nane pamoja na Spika wa bunge hilo kutokana na huduma na juhudi zao kubwa za kulitumikia taifa.
Hivi sasa tumeingia katika kipindi cha Bunge la Tisa. Nasaha zangu kubwa kwa wawakilishi na wabunge wapya ambao wamefika katika sehemu hiyo nyeti mno (Bungeni) kwa kura za wananchi, ni kwamba wanapaswa kufikiria tu majukumu yao mbele ya Mwenyezi Mungu na watekeleze vilivyo jukumu zito la ubunge na uwakilishi wa taifa, na wajiepushe kikamilifu na misukumo binafsi na pia waniweke mbali na kupenda na kukasirika kwa kuzingatia manufaa binafsi, au maslahi ya kundi fulani, au ya tabaka fulani au ya manufaa ya eneo fulani tu katika kutunga kwao sheria - ambalo ndilo jukumu kubwa zaidi ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu - na vile vile katika kusimamia utekelezaji wa sheria na tab'an pia katika uchukuaji misimamo na maamuzi ambayo yana athari za moja kwa moja kwa anga inayotawala nchini. Sheria iko juu ya mambo yote hayo. Sheria inapaswa kuwa yenye manufaa, inayokwenda na wakati, iwe wazi na yenye kuzingatia mahitaji ya umma na kudhamini manufaa ya taifa. Katika muongo huu wa maendeleo na uadilifu wa (Jamhuri ya Kiislamu ya Iran), sheria zote za muongo huu zinapaswa kulenga kufanikisha mambo hayo mawili (maendeleo na uadilifu) na inabidi sheria zote zitungwe kwa muono mpana wa hali ya juu ili ziweze kukusanya mambo mengi, ziwe pana, ziweze kutumika muda mrefu zaidi na katika mambo mengi zaidi. Inabidi vipaumbele vya nchi vitathminiwe, vijulikane vizuri na vipewe umuhimu unaotakiwa katika utungaji sheria.
Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu, ni moja ya nguzo kuu za nchi na za mfumo wa Kiislamu nchini Iran. Sifa zote kubwa na muhimu ya Jamhuri za Kiislamu zinapaswa kuakisiwa na kuonekana wazi katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu; imani, ushujaa, kuwa mstari wa mbele, kusimama kidete juu ya misingi ya Mfumo, kusimama imara mbele ya maadui, ubunifu na kwenda na wakati, umoja na mshikamano wa taifa, kazi, idili na kujitolea katika njia ya haki pamoja na kuingiza katika medani uwezo wote wa watu binafsi na wa jamii nzima kwa pamoja na hayo ni miongoni mwa mambo ambayo yanaweza kuifanya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu kuwa Bunge bora na la kupigiwa mfano.
Kuwepo ushirikiano wa kweli na uliojaa mapenzi baina ya Bunge na Mihimili Mikuu mingine na kujiweka mbali na mivutano isiyo na sababu ni sifa nyingine muhimu na yenye umuhimu mkubwa katika kuleta umoja na mshikamano wa taifa jambo ambalo mara zote limekuwa likisisitiziwa sana na watu wenye uchungu na nchi na wanaopigania manufaa ya umma na ambao wanaamini kuwa jambo hilo ndilo linaloweza kuliletea hadhi na heshima taifa la Iran kwa walimwengu. Nasaha hizi aidha, nazitoa kama zilivyo pia kwa Mihimili Mikuu mingine nchini na kwa watu na asasi zote husika. Kila mtu anapaswa kuifanya sheria kuwa kauli ya mwisho (sheria inapoamua, mtu hana njia nyingine ila kutii).
Katika duru zilizopita za Bunge niliwahi kutoa nasaha mbalimbali kwa waheshimiwa Wabunge na kuwakumbusha wajibu na majukumu yao mbele ya Mwenyezi Mungu katika dunia hii inayopita haraka kama ambavyo niliwakumbusha pia uadilifu usio na chembe ya shaka wa Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama. Hivi sasa pia narejea tena kutoa nasaha hizi kwenu waheshimiwa Wabunge kwa ikhlasi na udhati wa moyo wangu.
Mwisho namalizia kwa kumuombea rehema na amani Mtume wetu mtukufu SAW na Mitume wengine wa Mwenyezi Mungu na Maimamu watoharifu AS na kwa Imam wa Zama, Imam Mahdi (roho zetu ziwe fidia kwake) nikiziombea dua za kheri pia roho safi za mashahidi na roho toharifu ya Imam wa mashahidi. Aidha ninamuomba Mwenyezi Mungu akupeni nyote taufiki, uongofu na msaada Wake.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullah
Sayyid Ali Khamenei,
7/Khordad 1391 (Hijria Shamsia)
(27/Mei/2012 Milaadia).
captcha