Mohammad Morsi, mgombea kiti cha urais, katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais nchini Misri, kwa tikiti ya Ikwanul Muslimin ametoa wito wa kuunda harakati ya kitaifa dhidi ya hasimu wake, Ahmad Shafiq ambaye ni kati ya mabaki ya utawala wa dikteta aliyetimuliwa Husni Mubarak.
Kwa mujibu wa gazeti la Al Youm al Sabie la Misri, Morsi ameongeza kuwa katika duru ya pili ya uchaguzi utakaofanyika Juni 16 na 17 Wamisri wanapaswa kuungana dhidi ya mabaki ya Mubarak.
Wakati huo huo Bodi ya Wadhamini wa Mapinduzi ya Misri imetangaza kuwa itamuunga mkono mgombea wa harakati ya Ikhwanul Muslimin Muhammad Mosri katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais wa Misri itakayofanyika Juni 16 na 17 nchini humo.
Bodi hiyo aidha imeyataka makundi, wanaharakati na vyama vya kisiasa na vya kimapinduzi vya Misri kuweka kando hitilafu zao na kupiga hatua mpya katika kufanikisha malengo ya mapinduzi ya nchi hiyo.
Aidha Bodi ya Wadhamini wa Mapinduzi ya Misri imesisitiza makundi na mirengo inapaswa kuungana katika suala la kumuunga mkono Mohammad Morsi kwani huyo ndiye mgombea pekee wa mrengo wa Kiislamu katika duru ya pili ya uchaguzi wa Rais wa Misri na kwamba hatari inayoyakabili mapinduzi hayo haitaondoka hadi pale Morsi atakapooshinda katika duru ya pili ya uchaguzi huo.
1017598